Post Details

MAHAKAMA YAWEKA HISTORIA MPYA KATIKA MFUMO WA UTOAJI HAKI NCHINI

Published By:faustine.kapama

Na Faustine Kapama-Mahakama

Mahakama ya Tanzania imekamilisha ujenzi wa mfumo wa kunukuu na kutafsiri mienendo na hukumu, hatua inayokwenda kuongeza kasi na  uwazi wakati wa usikilizaji wa mashauri na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama.

Hayo yamebainishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika hotuba yake aliyoitoa kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma hivi karibuni.

Mhe. Prof. Juma ameeleza kwenye hotuba hiyo kuwa Mahakama ya Tanzania imekuwa ikitafuta mfumo (software) unaotumia akili bandia (Artificial Intelligence) kutafsiri mienendo ya mashauri na hukumu za Mahakama kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza.

“Tuligundua kuwa Mahakama ya Juu ya India tayari ilikuwa inatumia software hiyo kutafsiri lugha kubwa tisa za India na kubaini kuwa India walipata ujuzi huo kutoka Italia, nchi yenye utaalamu na uzoefu mkubwa wa kutengeneza programu au softaware za kutafsiri na kuweka sauti katika maandishi (translation and transcription),” ameeleza.

Jaji Mkuu amesema kuwa wataalamu wa Mahakama ya Tanzania, Mahakama Kuu Zanzibar, wakishirikiana na wale wa Serikali Mtandao (eGA) walikwenda Italia kutafuta na kufanikiwa kutengeza mfumo na kuufundisha lugha ya Kiswahili kwa lafudhi na sauti mbalimbali za Kitanzania. Ameeleza mfumo huo umejengwa kwa pamoja kati ya Mahakama ya Tanzania na Mkandarasi Almawave S.P.A wa Italia kwa kutumia fedha za ndani.

“Utakapoanza kutumika mfumo huu utawaondolea Majaji na Mahakimu jukumu zito la kunukuu na kutafsiri mienendo ya mashauri, hivyo kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri, uwazi na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama. Tanzania pia itapata mrahaba wa asilimia 20 kwa mauzo yoyote ya mfumo huu kwa mtu mwingine,” Jaji Mkuu amesema.

Alitumia fursa hiyo kutambua uwezeshwaji mkubwa kwa Mahakama uliofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa mwaka 2022 aliendelea kuiongezea nguvu kazi Mahakama kwa kuteua Majaji 22 wa Mahakama Kuu.

Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa uteuzi huo uliofanyika tarehe 6 Agosti, 2022 uliongeza idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu kutoka 78 hadi 100 na hivyo kupunguza mzigo wa mashauri kwa ngazi hiyo kutoka mashauri 340 hadi 265 kwa wakati huo.

Amebainisha pia kuwa kwa mwaka 2022, watumishi 292 wapya waliajiriwa, wakiwemo Mahakimu Wakazi 48, ongezeko lambalo limesaidia pia Mahakama kutimiza mpango wake wa kusogeza huduma zake karibu na wananchi kwa kuanzishwa kwa huduma ya Mahakama Kuu katika Mkoa wa Manyara na huduma za Mahakama katika Wilaya 12 kufuatia kukamilika kwa mradi wa majengo ya Mahakama za Wilaya.

“Uwezeshaji mkubwa ulifanyika katika miundombinu ya majengo. Katika kipindi cha mwaka jana 2022 Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa majengo mapya 32 yakijumuisha majengo 24 ya Mahakama za Wilaya na matano ya Mahakama za Mwanzo. Aidha, majengo mengine matatu ya Mahakama yamefanyiwa ukarabati mkubwa,” alisema.

Jaji Mkuu ameeleza pia kuwa ili kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi, kupitia mradi wa maboresho 2020/21- 2024/25, Mahakama inatarajia kufikisha huduma ya Mahakama Kuu katika mikoa nane isiyo na huduma hiyo ambayo ni Singida, Pwani, Songwe, Katavi, Geita, Njombe, Simiyu na Lindi.

Aidha, alisema, Mahakama inatarajia kujenga Mahakama za Mwanzo 60 na Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki 10, kikiwemo Kituo kimoja kitakachojengwa huko Pemba na kupitia fedha za ndani kutajengwa jumla ya majengo 24, kati ya hayo 14 ni ya Mahakama za Wilaya na 10 ni ya Mahakama za Mwanzo.

Mhe. Prof. Juma kipekee amemshukuru Rais Samia pamoja na Serikali yote anayoiongoza kwa kuridhia na kufanikisha Serikali kuingia katika makubaliano na Benki ya Dunia mwishoni mwa Februari 2022 ya kuongeza fedha na muda wa utekelezaji wa mradi huo wa maboresho.

“Kukamilika kwa majengo hayo kutaongeza pia mahitaji ya watumishi. Ni matumaini yangu kwamba Serikali itaendelea kuiwezesha Mahakama kwa kutoa vibali vya ajira ili kusaidia wananchi kupata huduma za Mahakama karibu na maeneo yao kwa gharama nafuu na kwa wakati,” amesema.

Watanzania waliadhimisha Siku ya Sheria tarehe 1 Februari, 2023 kama ishara ya kuanza mwaka mpya wa shughuli za kimahakama kote nchini. Maadhimisho ya kitaifa yalifanyika jijini Dodoma, ambayo ni Makao Makuu ya nchi na mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Comments (0)

Leave a Comment