Post Details

JAJI KIONGOZI AMALIZA ZIARA YA UKAGUZI KANDA YA DAR ES SALAAM

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama Morogoro

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amemaliza ziara yake ya siku tano kwa Kanda ya Dar es salaam na kuwataka watumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia maadili na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro pamoja na Mahakama za wilaya za Morogoro na Mvomero, Jaji Kiongozi amewakumbusha watumishi hao kutekeleza wajibu wao huku wakichukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona.

Alisema Mahakama itaendelea na huduma zake za utoaji haki licha ya kuwepo kwa ugonjwa huo isipokuwa imejipanga pia kutoa huduma hizo kwa njia ya Tehama. Aliongeza kuwa katika kukabiliana na Corona, watumishi hawana budi kuzingatia maelekezo yanayotolewa ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka mara kwa mara.

Ziara ya Jaji Kiongozi imethibitisha kutekelezwa kwa maelekezo ya wataalamu wa Afya ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa katika kupambana na Corona ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwa vifaa vya usafi kama maji tiririka, sabuni tishu pamoja na vitakasa mikono katika Mahakama zote.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Abeesiza Kalegeya alisema hatua nyingine zilizochukuliwa ni kupunguzwa kwa misongamano na mikusanyiko ya watu Mahakamani baada ya kuwekwa utaratibu wa kupunguza idadi ya watu wanaoingia Mahakamani. Hivi sasa wanaoruhusiwa kuingia ni wadaawa/washtakiwa wa kesi, mashahidi, Mawakili, Polisi pamoja na wadau wengine wa Mahakama wanaohitaji huduma muhimu.

Kuhusu ufunguaji wa  mashauri, Mhe. Kalegeya alisema mashauri yanayofunguliwa ni yale ambayo upelelezi umekamilika. Kwa upande wa usikilizwaji wa mashauri ambayo Mahakama ya Hakimu Mkazi na wilaya hazina mamlaka nayo na upelelezi haujakamilika, yanaahirishwa kwa mwezi moja. Pia mahabusu hawaletwi mahakamani isipokuwa wale ambao mashauri yao yapo hatua ya usikilizwaji. Kwa mashauri ambayo washtakiwa wapo nje kwa dhamana, kipaumbele kimewekwa kwa yale yaliyokaa mahakamani kwa muda wa zaidi ya miezi 12.

Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo, Mahakama hivi sasa zimeweka utaratibu wa kuweka masharti nafuu ya dhamana kwa washtakiwa ili kuwezesha kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.

Katika ziara yake, Jaji Kiongozi pia alikagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama inayoendelea katika kanda ya Dar es salaam. Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vinavyojengwa Kinondoni, Temeke, na Morogoro.

Mahakama ya Tanzania imeanza ujenzi wa vituo Jumuishi vya Utoaji haki sita katika miji ya Arusha, Mwanza, Dar es salaam, Dodoma na Morogoro. Vituo hivyo vinavyotarajiwa kukamilika ndani ya miezi kumi vitajumuisha Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za wilaya na Mahakama za Mwanzo na Ofisi za Wadau ndani ya jengo moja. Lengo ni kurahisisha huduma za utoaji haki na kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi.

 

Comments (0)

Leave a Comment