Post Details

MAJAJI MOROGORO UTAWAPENDA

Published By:faustine.kapama

  • Waanza kazi kutoa elimu ya kisheria kwenye vyombo vya habari

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe tarehe 23 Januari, 2023 amezindua utoaji elimu ya sheria kwenye Vyombo vya Habari huku akisisitiza wananchi kuendeleza imani yao kwa Mahakama ili iweze kuwatatulia migogoro waliyonayo.

Katika uzinduzi huo, Jaji Ngwembe aliambatana kwenye Kituo cha Redio Abood na Majaji, Mhe. Messe Chaba na Mhe. Gabriel Malata pamoja na viongozi wengine waandamizi, Naibu Msajili, Mhe. Augustina Mbando na Mtendaji wa Mahakama Bw. Ahmed Ng’eni.

Akizungunza kupitia Kituo hicho, Mhe. Ngwembe aliwasihi wananchi kujitokeza kufuatilia vipindi vya elimu vitakavyokuwa vikiendelea kutolewa kupitia Radio na Televisheni mkoani Morogoro kwani wameandaa mada zitakazowasaidi kuijua sheria na kuepuka makosa yatokanayo na kutoijua sheria.

Aliendelea kusisitiza wananchi kuishirikisha Mahakama ili kutatua migogoro yao kwakuwa watatumia usuluhishi kwa kipindi chote, hoja ambayo iliungwa mkono na Jaji Malata ambaye alielezea namna Kanda hiyo ilivyotumia usuluhishi kutatua mgogoro ulioendelea ndani ya familia kwa zaidi ya miaka ishirini.

“Baada ya kuwasuluhisha wote walitoka mahakamani wakiwa na furaha na kuahidi watakapofika nyumbani watapika chakula na kula kwa pamoja, hivyo unaweza kuona namana usuluhishi ulivyorejesha amani ndani ya familia hiyo,” alieleza Mhe. Malata.

Kwa upande wake, Mhe. Chaba alienda mbali zaidi na kufafanua kuwa njia ya usuluhishi ikitumika itampunguzia mwananchi gharama za kufika mahakamani na huokoa muda ambao utamsaidia kujikita katika shughuli za uzalishaji. Jaji Chaba aliwasihi wananchi kuendelea kuiamini Mahakama na kuleta mashauri yao ili yapatiwe ufumbuzi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.)

Comments (0)

Leave a Comment