Post Details

SHANGWE KILA KONA MAHAKAMA IKIADHIMISHA UZINDUZI WIKI YA SHERIA

Published By:faustine.kapama

Na Waandhishi Wetu-Mahakama ya Tanzania

Mahakama ya Tanzania imeadhimisha uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika Kanda na Mikoa mbalimbali nchini, huku wananchi na watumishi wakijitokeza kwa wingi. Kitu cha kipekee kimefanyika katika Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara kwa kufanya uzinduzi kupitia Mkutano Mtandao, njia ambayo haijawahi kutokea katika historia ya Mahakama nchini.

Mwandishi wetu Richard Matasha kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara, anaripoti kuwa jana tarehe 23 Januari, 2023 umefanyika uzinduzi wa Wiki ya Sheria kwa njia ya kipekee ya Mkutano Mtandao (Video Conference).

Watumishi pamoja na wadau katika maeneo mbalimbali ndani ya Kanda ya Mtwara inayojumuisha Mikoa miwili ya Lindi na Mtwara, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, walishiriki uzinduzi kwa njia hiyo kikamilifu.

Shughuli za uzinduzi zilianza kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Zainab Muruke kuwakaribisha wageni pamoja na Waandishi wa Habari kisha akaelezea kauli mbiu ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2023.

Katika hafla hiyo, kivutio kikubwa kilikuwa ni utambulisho wa kipekee wa mzee Issa Mohamed Mkumba (61), mkazi wa Kijiji cha msimbati wilayani Mtwara, ambaye anasifika kwa umaarufu wake katika masuala ya usuluhishi. (Taarifa zaidi kuhusu mzee huyu zitawaajia hivi punde).

Baada ya kutoa muhtasari juu ya kauli mbiu, Jaji Muruke alimkaribisha mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kutoa salamu zake kisha kumwalika Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Ahmed Abbas kuzindua maadhimisho ya Wiki ya Sheria katika Kanda hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa huyo alipongeza utaratibu mzuri wa kutumia TEHAMA katika uzinduzi huo na kuahidi kumtembelea Mzee Mkumba anayejulikana kama bingwa wa utatuzi wa migogoro.

Kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Paul Pascal anaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu aliwaomba wadau wa Mahakama kuweka mifumo mizuri ili kuhamasisha utatatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, kwani hakuna Mkoa wenye migogoro mingi kama Kilimanjaro, hasa inayohusu ardhi.

“Lakini pia nitoe rai kwa watumishi na watendaji wa Mahakama kujiepusha na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili na kuacha kufanya kazi kwa mazoea, wahudumieni wale wanaohitaji haki kwa weledi,” alisisitiza.

Mkuu wa Mkoa huyo aliwahimiza wananchi kujitokeza katika Wiki ya Sheria ili kupata msaada na ushauri wa kisheria, hivyo kuweza kutatua migogoro inayowakabili kwa njia ya usuluhishi.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Juliana Massabo alisema katika Wiki ya Sheria watatoa huduma mbalimbali kwa wananchi, ambapo watumishi na wadau wa Mahakama wamejipanga vyema kutekeleza jukumu hilo.

Jaji Mfawidhi huyo aliwaomba wananchi wote kwa makundi mbalimbali ya kijamii kushirikiana kwa pamoja ili kuifanya kauli mbiu ya mwaka 2023 kuwa ya vitendo kwani itasaidia kukuza amani, kupunguza mlundikano wa mashauri na kuondoa au kupunguza gharama za uendeshaji.

Naye Charles Ngusa kutoka Mahakama Geita anaripoti kuwa Wiki ya Sheria ilizinduliwa kama ilivyo kwa nchi nzima kwa kuanza na maandamano yaliyojumuisha watumishi, wadau mbalimbali pamoja na wananchi ambao wote walishiriki kikamilifu.

Maandamano hayo yalipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita. Mhe. Wilson Shimo akiwa pamoja na mwenyeji wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Cleofas Waane.

Wakati anamkaribisha Mkuu wa Wilaya, Mhe. Waane aliwakaribisha wananchi wote kufika katika vituo vilivyoandaliwa ili waweze kunufaika na elimu itakayotolewa katika Wiki ya Sheria nchini.

“Leo ni siku nzuri na maalumu kwa ajili ya wananchi na wadau wa sheria wote mkoani Geita ambayo sasa inafungua fursa kwa wote kuweza kupata elimu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria,” alisema.

Akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “Umuhimu wa utatuzi wa Migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu: Wajibu wa Mahakama na wadau”, Mhe. Waane alibainisha kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi unatambulika kisheria, huchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha amani na mahusiano.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, akizungumza katika hafla hiyo, aliipongeza Mahakama kwa kudumisha maazimisho hayo kila mwaka ambapo wananchi hupata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ya kisheria.

Alisema kuwa uwepo wa Wiki ya Sheria hukumbusha kila mwananchi kwamba hakuna aliye juu ya sheria na Mahakama ndiyo chombo pekee kilichoidhinishwa kikatiba kutoa haki.

Mhe. Mkuu wa Wilaya amesisistiza na kuwaomba wananchi wote kuitumia fursa hiyo kupata elimu ya kisheria. “Tunapaswa kuitumia vyema fursa hii ili tuweze kujifunza kupitia vituo hivi na jambo zuri ni kwamba wanaotoa elimu katika wiki hii ndiyo wale wanaotoa tafsiri ya sheria, hivyo tuitumie fursa hii,” alisisitiza.

Akielezea kauli mbiu ya mwaka huu, Mkuu wa Wilaya huyo alisema kuwa imebeba ujumba muhimu kwa kuwa inakumbusha kusuluhisha migogoro kwa kukaa pamoja bila kufika mahakamani, hivyo kuipunguzia Mahakama mlundikano wa mashauri.

Mhe. Shimo alitumia fursa hiyo kumshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kuweka mpango wa kuanzisha Mahakama Kuu katika Mkoa wa Geita kwani itasaidia kuwapunguzia wananchi gharama za kuifuata huduma hiyo katika Mkoa wa Mwanza.

Ameomba kama ikiwezekana huduma ya Mahakama Kuu ianze hata kabla ya jengo linalotarajiwa kujengwa kwa kupitia majengo mengine na yeye mwenyewe.

Kwa upande wake, James Kapele – Mahakama Katavi anaripoti kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi imezindua Wiki ya Sheria kwa mwaka 2023 huku mgeni maalum, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Pesambili Simuyemba akifurahishwa na kauli mbiu ambayo imekuja kwa muda muafaka hasa ukizingatia kuwa Mkoa wake unayo migogoro mingi ya ardhi inayohitaji usuluhishi zaidi ili iweze kumalizika haraka, hivyo kuruhusu wadau kuendelea na shughuli za kilimo.

“Naipongeza sana Mahakama kwa kutuletea kauli mbiu hii inayoosisitiza umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumu endelevu. Kauli mbiu hii ni ya kimkakati kwa kuwa itachangia sana kumaliza migogoro mingi hasa ya ardhi ambayo ni mingi hapa mkoani kwetu. Mkoa wetu ni wa kilimo, hivyo kumalizika kwa migogoro kwa njia ya usuluhishi itakuza uchumi,” alisema.

Aidha, amemtaka Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mpanda Mhe, Gregory Rugalema kukutana na wenyeviti wa mabaraza yote ya ardhi mkoani Katavi ili kuweza kuweka mipango mahsusi kuona ni kwa namna gani kuli mbiu hiyo itawasaidia kupunguza migogoro ya ardhi.

Awali akitoa salamu zake za ufunguzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye amefafanua kwa kina maudhui ya kauli mbiu hiyo kwa kuzielezea faida nyingi za kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi. Amesistiza pia kwa kuwataka wadau hasa Mawakili kuwa mstari wa mbele katika kuisimamia kauli mbiu hiyo kwa kuwa wao pia wamekuwa vinara wa kukwamisha usuluhishi pindi shauri linapokuwa linahitaji kumalizika kwa njia hiyo.

“Kauli mbiu hii ni muhimu sana kwa dunia ya sasa kwani kama mashauri mengi ambayo sheria zinaruhusu tuyamalize kwa njia ya usuluhishi yatakuwa na faida nyingi ikiwemo kuwa na jamii yenye amani, kupunguza mlundikano mahakamani, kuimarisha uchumi wa watu wetu na mengine mengi. Tatizo linabakia kwenu hasa Mawakili ambao mara nyingi mkienda kwenye usuluhishi mnarudi kusema umeshindikana,” alisisitiza.

Naye Amani Mtinangi kutoka Mahakama Kuu Tabora anaripoti kuwa maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2023 yalifunguliwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Dkt. Balozi Batilda Buriani. Sherehe za ufunguzi zilitanguliwa na matembezi kutoka Viwanja vya Mahakama Kuu hadi viwanja vya Chipukizi vitakavyotumika kutoa elimu ya sheria kwa muda wa wiki nzima.

Wadau mbalimbali walishiriki katika matembezi hayo, wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu, Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa, Mawakili wa Serikali na wale wa kujitegemea, Wanafunzi, Taasisi binafsi na umma pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Amour Khamis alieleza kuwa kufunguliwa kwa shughuli hiyo kunaashiria kuanza rasmi zoezi la utoaji elimu kwa umma ambayo ni sehemu muhimu katika maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria nchini.

Alieleza kuwa wadau wote wamejipanga vyema kutoa elimu kwa njia ya Vyombo vya Habari, mihadhara mashuleni, makanisani, misikitini, magereza na katika maeneo mengine, hivyo wananchi wawe tayari kupata elimu kwa kipindi chote.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa matembezi hayo yameamsha hamasa kwa wananchi kujua umuhimu wa Wiki ya Sheria, hivyo akaipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa ushirikishaji mkubwa wa wadau katika shughuli nzima ya utoaji haki.

Alitoa wito kwa wananchi wote wa Tabora kufika kwa wingi katika viwanja vya Chipukizi ili kupata elimu juu ya taratibu mbalimbali za kimahakama, kwani Mahakama na wadau wake wamejipanga kikamilifu kutoa elimu ya masuala mbalimbai yahushuyo sheria.

Mhe. Dkt Buriani alieleza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inakumbusha kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ni njia pekee itakayo punguza matumizi mabaya ya rasilimali kama mashauri siyo lazima kufikishwa mahakamani.

Kutoka Mahakama Tanga, Mwandishi wetu Mussa Mwinjuma anaripoti Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Omari Mgumba aliongoza matembezi maalum kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini.

Kuelekea kuanza kwa mwaka mpya wa shughuli za Mahakama kote nchini, Mahakama Kanda ya Tanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imejipanga kutoa elimu bure kwa wananchi katika Wiki ya Sheria ili kuongeza uelewa na kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili.

Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka 2023 imebebwa na kauli mbiu isemayo “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi katika Kukuza Uchumi Endelevu:   Wajibu wa Mahakama na Wadau.”

(Habari hizi zimekusanywa na kuhaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

Comments (0)

Leave a Comment