Published By: | kansha.innocent |
---|
Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma
Ikiwa ni siku ya tatu toka kuzinduliwa rasmi kwa maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya utoaji elimu ya sheria nchini na mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma mnamo tarehe 22 Januari, 2023, Mahakama ya Tanzania pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya sheria nchini wamendelea kuwapokea wananchi na kutoa elimu ya masuala mtambuka ya kisheria kwa wadau wa Mkoa Dodoma na viunga vyake.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la kupata elimu Bw. Iddris Haji Chukwepe mkazi wa Veyula jijini hapa amesema, utaratibu huo wa kutenga muda maalumu na kuwapa wananchi elimu ni mzuri sana na unalenga kupunguza malalamiko yatokanayo na ukosefu wa elimu ya sheria na kupunguza migogoro isiyo ya lazima katika jamii.
“Binafsi nimefurahishwa sana mimi kama mfanyabiasha mdogo (mmachinga nilivunjiwa kibanda changu cha biashara na mgambo wa Jiji eti kwa amri ya Mkuu wa Wilaya, sikujua nianzie wapi kudai haki yangu lakini niliposikia matangazo ya siku ya sheria, leo nimefika banda la malalamiko la Mahakama na kuelekezwa utaratibu mzima wa namna ya kudai mali zangu zilizopotea kwa lugha nyepesi na laini”, alieleza Bw. Chukwepe.
Akatoa rai kwa Muhimili wa Mahakama na wadau wa sekta ya sheria nchini kuwa elimu hiyo yenye manufaa kwa wananchi isihishie katika wiki ya sheria bali elimu hiyo iendelee kutolewa hasa maeneo ya vijijini waliko wananchi wengi wazalisha mali, alisisitiza Chukwepe.
Mwananchi huyo anatukumbusha kurejea Nukuu ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliyoitoa mbele ya Mgeni rasmi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango siku ya uzinduzi.
Ananukuu “Ningependa kuchukua muda huu kuwaomba wananchi ambao wanataka kudai haki zao au wanataka kufahamu haki zao, hatua ya kwanza kabisa ya kuidai haki yako ni kuifahamu wewe mwenyewe.
"Kuifahamu kwa kusoma, kutafuta elimu ya kuweza kukuwezesha kujua shughuli zako zinaongozwa na sheria ipi na kwa utaratibu upi hiyo ndiyo hatua ya kwanza kabisa, kabla hata hujamtafuta mwanasheria au ndugu na jamaa akusaidie. Wewe mwenyewe fanya juhudi za kufahamu hizi shughuli ninazofanya zinaongozwa na sheria ipi, zinaongozwa na utaratibu upi alafu endelea na kufanya kazi.”
Mwananchi huyo anaendelea kumnukuu Jaji Mkuu ambaye aliendea kusema, "Hii ardhi ninayonunua inaongozwa na sheria ipi, mipaka yake ikoje kwa hiyo ukiwa katika ufahamu huo utakuwa katika ufahamu mzuri sana utakuwa katika nafasi nzuri sana ya kuzipigania haki zetu na vilevile kuhakikisha kwamba hiyo haki unaipata kwa urahisi zaidi.”.