Post Details

JAJI KIONGOZI: CORONA ISIWE KIKWAZO HUDUMIENI WANANCHI KWA TAHADHARI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Mahakimu na Watumishi wa Mahakama kwa ujumla kuendelea kuhudumia wananchi licha ya changamoto ya janga la Ugonjwa wa ‘Corona’ unaoendelea kutikisa dunia kwa sasa.

Akizungumza kwa nyakati tofauti alipotembelea Mahakama kadhaa jijini Dar es Salaam, Machi 31, 2020, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi alisema kuwa kila Hakimu ajikumbushe wajibu wake kwa kusoma vifungu 107A na B vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vilevile wakumbuke kusimamia viapo vyao.

“Kipindi kama hiki hakisimamishi migogoro kutokea kwenye jamii, hivyo ni lazima kazi zifanyike, ni kipindi ambacho kinatukumbusha ni namna gani bora zaidi ya kuboresha huduma ya utoaji haki nchini,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.

Mhe. Jaji Kiongozi aliongeza kwa kuwataka Watumishi hao kuwa wabunifu katika maeneo yao ya kazi na kutokubweteka kwa kusikiliza idadi chache ya mashauri kwa Mahakama ambazo zina idadi chache ya mashauri na kuwataka kutosita kudai nyongeza ya idadi ya mashauri ya kuyafanyia kazi endapo waliopangiwa na Wafawidhi wao ni machache.

Aidha; Mhe. Jaji Dkt. Feleshi aliwataka Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya ya Kigamboni, Temeke na Ilala kuendelea kuboresha ushirikiano na Wadau wa Mahakama katika suala zima la kuhakikisha kuwa haki inatolewa kwa wakati.

Mhe. Jaji Kiongozi amefanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama katika Mahakama za Wilaya za Kigamboni, Temeke na Ilala, Mahakama za Mwanzo za Temeke, Mbagala, Ukonga, Buguruni na Ilala na amefanya ukaguzi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha utoaji haki kinachojengwa Chang’ombe wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo; Mhe. Jaji Kiongozi amewasifu Wafawidhi na Watumishi wote wa Mahakama alizotembelea kwa kuunga mkono jitihada za Viongozi Wakuu wa Mahakama za kuhakikisha kuwa huduma za haki nchini inatolewa kwa ubora kwa wananchi wote.

Mhe. Jaji Kiongozi aliwataka baadhi ya Watendaji wa Mahakama alioambatana nao kushughulikia changamoto zote zilizoibuliwa katika ziara yake ambazo ni pamoja na uhaba wa watumishi kwa baadhi ya Mahakama hasa Kada za Wasaidizi wa Ofisi, Mlinzi na Makarani, ufinyu wa bajeti na kadhalika.

Msimamizi huyo wa Mahakama Kuu na Mahakama za chini anatarajia kuendelea na ziara yake ya Kanda ya Dar es Salaam ambapo atatembelea pia Pwani na Morogoro lengo ni kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa huduma ya utoaji haki pamoja na kuangalia ni kwa jinsi gani Kanda hii inachukua tahadhari za mapambano dhidi ya janga la ‘Corona’ katika kuhakikisha usalama wa Watumishi na wateja wa Mahakama.

Comments (0)

Leave a Comment