Post Details

MAHAKAMA KUTUMIA TEHAMA KUPAMBANA NA VIRUSI VYA CORONA

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama

Mahakama ya Tanzania imeongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake ili kuzuia kuenea kwa Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona na pia kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika kupambana na ugonjwa huo.

Akizungumza na Waandisi wa Habari jijini Mwanza, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Mahakama imeongeza maeneo ya matumizi ya Tehama katika kipindi hiki ambapo dunia inapitia wakati mgumu wa kupambana na virusi vya Corona ambavyo vimesambaa nchi nyiongi duniani.

“Mahakama imekuwa ikitumia Tehama katika kurahisisha shughuli zake za utoaji haki nchini licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa Corona na baadhi ya mifumo iliyokuwa ikitumika ni pamoja na  mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri pamoja na mfumo  wa kusikiliza mashauri kwa njia ya mkutano mtandao (Video Conferencing),” alisema Jaji Mkuu.

Alisema matumizi ya Tehama ndani ya Mahakama yanatokana na Mpango wa miaka mitano wa maboresho ya huduma za Mahakama ambapo maboresho hayo sasa yatatusaidia katika kukabiliana na kupambana na ugonjwa huu ambao umesambaa kwenye nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kupitia mifumo ya Tehama iliyopo Mahakamani, wananchi na wadaawa wa mashauri huweza kupata huduma za kimahakama bila ya kuwalazimu kufika mahakamani hivyo kutoa fursa kwao ya kutumia muda huo kufanya shughuli za nyingine za uzalishaji na za kijamii.  

Alisema ili kutekeleza azma yake ya kutumia Tehama, Mahakama imeweka mitambo ya kisasa ya Tehama kwenye Mahakama Kuu Masjala Kuu jijini Dar es salaam, Mahakama kuu za Mbeya na Bukoba, kwenye Kituo cha Mafunzo Kisutu, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto pamoja na kwenye magereza ya Keko na Segerea.  

“Hatua ya Mahakama iliyofikiwa katika matumizi ya Tehama itakuwa ni njia mojawapo itakayosaidia kukabiliana na maambaukizi ya virusi vya COVID 19 kwa kuwa itaondoa mikusanyiko kwenye maeneo ya Mahakama na wananchi kuendelea kupata huduma hizo kwa njia ya mtandao”.

Kwa sasa, mashauri yote ya jinai jijini Dar es salaam yanayoahirishwa kutokana na sababu mbalimbali, watuhumiwa waliopo katika magereza ya Keko na Segerea hawatalazimika kufikishwa mahakamani, badala yake mashauri hayo yataahirishwa kwa njia ya Mahakama mtandao ili kuepuka msongamano na mkusanyiko wa kuwaleta Mahabusu mahakamani.

Ili kupanua huduma ya Mahakama mtandao kwenye kanda nyingine za Mahakama Kuu ya Tanzania, vifaa vya kuwezesha huduma hiyo vitafungwa pia katika magereza yaliyopo kwenye maeneo hayo ili huduma hiyo pia ianze kutolewa. Juhudi za kuweka vifaa hivyo kwenye kanda nyingine zinaendelea na tunarajia baada ya muda mfupi huduma itatolewa kwenye maeneo hayo. Kanda zenye huduma hiyo ni Mbeya na Bukoba.

Akifafanua kuhusu kanuni za kufungua mashauri kwa njia ya mtandao, Jaji Mkuu alisema zilianza kufanya kazi April, 2018 na kuongeza kuwa kanuni hizi ni muhimu katika kufungua mashauri kwa njia ya mtandao hivyo zitasambazwa ili kuwasaidia wananchi na wadau kufungua mashauri bila ya kufika mahakamani.

Alitoa wito kwa wananchi kufungua mashauri kwa njia hii ili kupunguza mikusanyiko isiyokuwa na lazima hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya Corona.

Alisema Mahakama inawashauri wananchi, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa kujitegemea kutoa ushirikiano hasa upande wa mashauri ya madai kutumia njia hii ya kusajili online. Tunatarajia hivi karibuni, hata mashauri ya jinai yatasajiliwa kupitia mitandao itakayotayarishwa kwa ajili hiyo. Njia hii itawaondolea wananchi usumbufu wa kusafiri kufika mahakamani na kutumia muda huo kwa shughuli za uzalishaji na kijamii.

Aidha, Jaji Mkuu amewashauri Viongozi wote wa Mahakama katika ngazi zote   kutumia wakati huu kuonyesha uongozi wao kwa kuwasaidia watanzania kuendelea kupata huduma za utoaji haki katika dunia ambayo inapata msukosuko mkubwa wa ugonjwa wa Corona.

Hivi sasa Mahakama ina mifumo mbalimbali kama  Mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri, mfumo wa kusimamia mawakili, mfumo wa kuhifadhi maamuzi ya Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, mfumo wa video conferencing na mfumo wa utambuzi wa majengo ya Mahakama.

 

 

Comments (0)

Leave a Comment