Post Details

WASHIRIKI 49 WAJENGEWA UWEZO KURIPOTI HABARI ZA MAHAKAMA.

Published By:Mary C. Gwera

Jumla ya washiriki 49 kutoka mikoa mbalimbali nchini wameanza mafunzo ya siku tano yanayofanyika Mjini Morogoro kuanzia Machi 16 hadi 20, mwaka huu kwa lengo la kujengewa uwezo wa kuripoti habari zinazohusu Mahakama ya Tanzania kwa usahihi.

Mafunzo haya yanafanyika kwa makundi mawili tofauti ambayo ni Wahariri wa Habari (Sub Editors) pamoja na Maafisa wa Mahakama ambao ni wawakilishi wa Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Akifungua mafunzo hayo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Paul Kihwelo alisema Mahakama ya Tanzania inatambua mchango mkubwa wa wanahabari kama isemavyo nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa Miaka Mitano (2015/2016 hadi 2019/2020).

“Mahakama inatambua umuhimu wa habari na wanahabari na Maafisa Habari wa Mahakama wana nafasi kubwa ya kuieleza jamii mambo yanayoendelea mahakamani, sio tu kueleza mambo ya mahakama ila kueleza taarifa za Mahakama kwa usahihi,”. alisema Jaji Kihwelo.

“Mafunzo haya yaliwekwa kwa miaka miwili mfululizo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mpango huo, na hili ni eneo muhimu kupita nguzo ya tatu inayosisitiza Kujenga imani kwa wananchi na ushirikishwaji wa wadau katika mpango huu,” alisema Jaji Kihwelo.

Jaji Kihwelo alisisitiza kwamba mafunzo hayo yana lengo la kufanya tathimini ya mafunzo yaliyotolewa awali ili kujipanga kwa mafunzo yanayotolewa sasa na jinsi gani ya kujipanga vizuri kwa mafunzo yatakayofanyika baade.

Mahakama mara nyingi huzungumuza au kutoa maamuzi kupitia kalamu na Jaji au Hakimu hawezi kutoka mbele ya umma kutetea uamuzi wake kwa umma hii ni kutokana na mfumo wa kitaasisi, hii imekuwa na mijadala mingi sio kwa Tanzania tu hata duniani kote ndio inatufanya tuwe na Maafisa Habari ili waweze kutoa ufafanuzi wa hali kama hizi za sintofahamu, alifafanua Jaji Kihwelo.

Aidha, alisema kuwa watu wengi hawajui mifumo ya mahakama inavyofanya kazi kutoka ngazi moja kwenda nyingine. Hali inayosababisha wakati wanapokosoa kutofanya katika misingi iliyo sahihi, hivyo mafunzo haya yatasaidia kutengeneza njia bora ya kutatua changamoto kama hizo.

Comments (1)

  • Photo Loading... Prof. SAM

    Hongera sana kwa Mahakama ya Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika kujipambanua kwa Umma tofauti na ilivyokuwa awali. Hongera kwa Viongozi wote wa Mahakama ya Tanzania.

    24-03-2020

Leave a Comment