Post Details

BODI YA UDHAMINI WA TAARIFA ZA MAJUZUU YA SHERIA YAJIPANGA

Published By:Mary C. Gwera

Bodi ya Udhamini wa Taarifa ya Majuzuu ya Sheria imejipanga kukamilisha uchambuzi wa maamuzi ya Juzuu ya mwaka 2019 ifikapo Juni, 2020 na kukamilisha uchambuzi wa maamuzi ya Juzuu ya mwaka huu mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumza katika  kikao cha Bodi hiyo, kilichofanyika  katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sheria kwa Vitendo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Jacobs Mwambegele alisema lengo ni kuhakikisha  hadi kufikia mwaka 2021 Mahakama inaweza kutoa Majuzuu kwa awamu mbili au nne ndani ya mwaka mmoja wa fedha.   


“Bodi imekutana ikiwa tayari imeshaandaa maamuzi kwa ajili ya taarifa za majuzuu ya Sheria ya Mwaka 2007 hadi Mwaka 2017 na katika kikao hicho kuweza kukamilisha maamuzi kwa ajili ya Taarifa za Juzuu la Sheria la Mwaka 2018.  Majuzuu yote ya Taarifa za Sheria ambayo maamuzi yake tayari yameshachambuliwa yatakamilika baada ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania kukamilisha taratibu za kupata mzabuni wa kufanya kazi hiyo,” alisema Mhe. Mwambegele.

Bodi hiyo ya Majuzuu ya Sheria imemaliza kikao chake  cha siku mbili (2) Machi 11 mwaka huu cha kuchambua maamuzi ya Mahakama Kuu kwa upande wa Zanzibar  na  Mahakama ya Rufani Tanzania na hivyo kukamilisha kuandaa  Juzuu ya Taarifa za Sheria ya mwaka 2018.

Bodi hiyo ina jumla ya Wajumbe 12, ambao ni Majaji kutoka Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu Tanzania  Bara na Zanzibar, Wawakilishi wa Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali na upande wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa pande zote mbili, Katibu pamoja na Mratibu wa Bodi hiyo.

Comments (0)

Leave a Comment