Post Details

‘IJA’ YAWAANDAA MADALALI NA WASAMBAZA NYARAKA ZA MAHAKAMA

Published By:Mary C. Gwera

Jumla ya Washiriki 22 kutoka mikoa mbalimbali nchini wanashiriki katika Mafunzo ya kusajiliwa kama Madalali wa Mahakama na Wasambaza nyaraka za Mahakama ya Tanzania yanayotolewa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA).

Akizungumza wakati akifungua rasmi mafunzo hayo yanayofanyika katika Shule ya Sheria jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo cha ‘IJA’, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo alisema kuwa mafunzo haya ambayo ni ya awamu ya tano (5) kufanyika yamelenga kuwajengea uwezo washiriki wa namna ya kufanya kazi ya udalali na usambazaji wa nyaraka za mbalimbali za Mahakama.

“Mnamo mwaka 2017 kanuni mpya za kusimamia Kada ya Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama zilitungwa na kupitishwa na Mhe. Jaji Mkuu, miongoni mwa masuala yaliyopitishwa ni pamoja na kutenganisha kada hizi mbili ili kuleta ufanisi zaidi,” alieleza Mhe. Jaji Kihwelo.

Mkuu huo wa Chuo aliongeza kuwa lengo jingine la mafunzo hayo ni kuwawezesha washiriki hao kufanya mtihani ambao utawawezesha kupata cheti cha umahiri endapo watafaulu mtihani akisisitiza kuwa hii ni moja ya takwa la kanuni kwa washiriki hao kukubaliwa kufanya kazi hiyo.

Kwa mujibu wa Jaji Dkt. Kihwelo alisema kuwa tofauti na awali, kwa sasa yeyote anayetaka kufanya kazi hizi ni lazima awe na elimu ya angalau  kidato cha nne (4) na kuhudhuria Mafunzo yanayotolewa na Chuo hicho ili kupata hati ya umahiri ‘certificate of competence.’

Mafunzo hayo ya  siku 14 yamehudhuriwa na washiriki kutoka mikoa mbalimbali kama Mwanza, Bukoba, Geita, Arusha, Ruvuma, Shinyanga na Dar es Salaam na wanatarajia kupatiwa mada kadhaa na Naibu Wasajili na Mahakimu wenye uzoefu Mahakamani.

Katika Mpango Mkakati wa miaka mitano (5) wa Mahakama wa 2016/2017-2020/2021, miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na kuboresha shughuli za utoaji haki ili kujenga taswira chanya kwa jamii.

Katika kutekeleza azma nzima ya uboreshaji wa huduma ya utoaji haki nchini, kada ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza nyaraka za Mahakama ilizingatiwa kwa kuwa ni mojawapo ya makundi muhimu yanayotekeleza amri mbalimbali za Mahakama.

Comments (0)

Leave a Comment