Post Details

TAWJA YAELIMISHA WATOTO KUHUSU UKATILI WA KIJINSIA

Published By:LYDIA CHURI

Siku ya wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka nchini Tanzania na kwingineko ulimwenguni. Mwaka huu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) kimeanza maadhimisho hayo kwa kutoa elimu ya sheria kwa kuwalenga watoto wote ili wawe na ufahamu na masuala yanayohusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa kuzitembelea shule kumi za msingi zilizoko jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Joaquine De Mello, wameanza na shule kumi lakini mpango ni kuzifikia shule nyingi zaidi na elimu hiyo itakuwa ikitolewa wakati wa sherehe na maadhimisho mbalimbali iliwemo siku ya Mtoto wa Afrika.

Machi 6, 2020 wanachama wa TAWJA walitoa elimu katika shule kumi zilizopo kwenye wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo pamoja na Kigamboni. Yafuatayo yalijiri kwenye maeneo hayo.

Na Lydia Churi-ILALA

Mwenyekiti wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Joaquine De Mello amewataka wanawake wenye watoto kuchukua nafasi zao katika malezi ya watoto wao ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyowezesha kufanyiwa.

Akizungumza na watoto wa shule za Msingi za Ilala Boma na Mkoani zilizopo wilayani Ilala jijini Dar es salaam, Jaji De Mello alisema licha ya wanawake kuwa na majukumu mengi bado wanatakiwa kufahamu ni changamoto gani watoto wao wanapitia tangu wanapotoka asubuhi kwenda shule mpaka jioni wanaporudi.

Amewataka wanawake kuwa makini na watu wanaowazunguka watoto majumbani wakiwemo ndugu wanaoishi majumbani kwani tathmini ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia inaonesha kuwa watoto wengi hufanyiwa vitendo hivyo na ndugu waliopo majumbani. Vitendo hivyo ni pamoja na ubakaji, ulawiti kupigwa na kunyanyaswa.

Jaji De Mello pia aliambatana na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Rehema Mgonya na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmilla Sarwatt ambao pia walizungumza na watoto wa shule hizo na kuwataka kuwa makini na kufahamu sheria inayowalinda watoto (Sheria ya Mtoto) na pia kufahamu haki za msingi za watoto zikiwemo haki ya kuishi na kupata elimu.

Zaidi ya wanafunzi 1300 wa shule za Msingi za Ilala Boma na Mkoani walipatiwa elimu ya masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.

Na Magreth Kinabo-KINONDONI

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sophia Wambura amewataka wazazi na walezi waliowatelekeza watoto wao kuwajibika kuwatunza ili watoto hao waweze kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu, malazi na chakula.

Akizungumza baada kutoa elimu kwa wanafunzi 667 wa shule za msingi za Kinondoni na Msisiri, Jaji Wambura pia aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata pia elimu ya kidini  kwa lengo la kuwajenga kimaadili watoto hao.

Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Kinondoni, Joyce  Julias alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto watoto wa wilaya hiyo kuwa ni pamoja na  wazazi kutowajibika kimalezi, kuvunjika kwa ndoa hali inayosababisha  asilimia kubwa kulelewa na bibi zao au mzazi mmoja  na kuwepo kwa mazingira hatarishi na umasikini.  

Mwalimu huyo pia aliwataka wazazi na wazee wa kimila kuacha kuwafanyia tohara watoto wa kike kwa kuwa kitendo hicho ni ukatili wa kijinsia.

Majaji  na Mahakimu wanawake ambao ni wanachama wa chama cha Majaji na Mahakimu wanawake (TAWJA) walitoa elimu kwa wananfunzi kuhusu masuala ya kijinsia. Majaji hao ni kutoka Mahakama ya Rufani, ambao ni Mhe. Winfrida Korosso na Mhe. Barke Sehel, pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao ni Mhe. Sophia Wambura na Mhe. Dkt. Modesta Opiyo. Wengine ni baadhi ya  Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.

Na Innocent Kansha-TEMEKE

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Temeke Mhe. Mariam Mchomba amewataka watoto kutambua njia sahihi za kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya kikatili wanapofanyiwa.

Akitoa Elimu juu ya vitendo vya kikatili dhidi ya watoto katika Shule za Msingi za Umoja na Migurani Wilayani Temeke mkoani Dar es salaam, Hakimu huyo amezitaja baadhi ya sehemu watoto wanazopaswa kutoa taarifa endapo watafanyiwa vitendo hivyo kuwa ni kwa watoto wenzao, kwa marafiki, walezi, waalimu, makanisani, misikitini na mjumbe aliye karibu na mahali mtoto aliyefanyiwa ukatili anapoishi.

Mhe. Mchomba alisema ukatili dhidi ya mtoto ni hatari katika jamii endapo tabia kama hizi hazitakemewa kwa nguvu zote na kila mlezi, mzazi, jamii na serikali kwa ujumla kwa kuwa vitachangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili ya kizazi kijacho.

Naye, mtoa mada mwingine Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mwambao Bagamoyo Mhe. Mwanakombo Twalib aliwakumbusha watoto kutojiunga na kushiriki katika makundi mabaya ya kuvuta bangi, kunywa pombe na madawa ya kulevya, na vitendo vya ulawiti kwani havikubaliki katika jamii.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Umoja Salim Matibwa alitoa ufafanuzi juu ya aina ya kamati zilizoundwa shuleni za kupambana na ukatili dhidi ya Mtoto kuwa ni Kamati za Nidhamu, Wazazi, Watoto Tuseme, Kamati ya Ushauri nasaha hasa kwa wale watoto wenye matatizo ya malezi.

Mahakimu hao pia walitoa mada zilizowaelimisha watoto juu ya mambo mengine ikiwa ni pamoja na ukeketaji, mimba za utotoni, ajira na kazi nzito kwa mtoto, na vipigo vinavyopita kiasi kwa wazazi na walezi.

Kwa mujibu wa kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 Mtoto ni mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18. Sheria hii ya mtoto inakataza ubaguzi wa aina yeyote dhidi ya watoto.

Na Tawani Salum-KIGAMBONI

Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya amewataka watoto kutonyamaza wanapofanyiwa vitendo vya kikatili na badala yake watoe taarifa ili vitendo hivyo vikomeshwe.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa TAWJA waliokuwa wakitoa elimu kwa watoto wa shule za msingi za Vijibweni na Darajani zilizopo wilayani Kigamboni jijini Dar es salaam, Mhe.Nkya alisema endapo mtoto atanyanyaswa kijinsia anapaswa kutoa taarifa haraka iwezekanavyo.

Alifafanua kuwa shauri la aina hiyo linapofikishwa mahakamani, katika usikilizwaji wake, mtoto hataonyeshwa kwa watu ili kumlinda na pia hata  hukumu ya shauri hilo haitatolewa jina la mtoto husika. Aliwasisitiza watoto kutokaa kimya wanapofanyiwa ukatili kwani wakikaa kimya watu waofanya vitendo hivyo wataendela kufanya kwa kujua hakuna adhabu yoyote watakayopewa.

Aidha Mhe. Nkya pia aliwaelimisha watoto juu ya haki zao pamoja na wajibu wao kwa wazazi wao, aliwataka watoto wasikubali kuolewa chini ya umri wa miaka 18 hiyo ni haki yao kimsingi kwani wanatakiwa kusoma kwa bidii.

Naye Hakimu wa Mahakama ya Jiji Mhe. Hanifa Mwingira aliwataka watoto kutokubali kunyanyaswa kijinsia kwa kigezo cha kutoka katika familia maskini

Aliwaeleza watoto hao kutomwamini mtu yeyote na endapo wataona dalili za mtu kutaka kuwanyanyasa kijinsia wakimbie huku wakipiga kelele. Aliwataka kutokubali kuitwa majina kama mume, mke, baby na mengineyo na namna nyingine ya kujikinga ni kutopita vichochoni na kujiepusha na walevi.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Butamo Phillip amefurahishwa na elimu iliyotolewa na Chama cha Wanawake Cha Majaji na Mahakimu Tanzania katika shule za Msingi za Vijibweni na kusema elimu hiyo  imesaidia kuwapa ufahamu wanafunzi  ni jinsi gani ya kukabiliana na unyanyasaji wa jinsia na nini wakifanye mara ikitokea wamefanyiwa unyanyasaji huo.

Jumla ya wanafunzi 3,929 walipata elimu hiyo na hivyo kukamilisha dhana ya TAWJA ya kutoa elimu juu ya ukatili, unyanyasaji wa kijinsia kwa Watoto, wajibu wa Watoto kwa wazazi, sheria ya mtoto pamoja na Watoto kukinzana na sheria. Wanachama wa TAWJA waliotoa elimu ni Jaji Mhe. Butamo Phillip Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Masabo, Mhe. Eva Nkya. Wengine ni Mahakimu  Mhe.Hanifa Mwingira,  Mhe.Agness Mchome,  Mhe. Lusajo Mtuwa na baadhi ya Maafisa wa ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Kigamboni.

Comments (0)

Leave a Comment