Post Details

TANZANIA NCHI YA MFANO AFRIKA KATIKA MRADI WA MABORESHO

Published By:LYDIA CHURI

 Benki ya Dunia imeitaja Tanzania kuwa nchi ya kwanza na ya mfano barani Afrika katika kutekelezaji Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama na kuiongezea muda wa kutekeleza mradi huo kwa awamu ya pili itakayomalizika mwaka 2025.

Mahakama ya Tanzania ilianza kutekeleza Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kipindi ambacho kitamalizika mwaka 2021. Aidha, awamu ya pili ya mradi huo inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2024/2025. 

Miongoni mwa maboresho yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania kupitia Mradi huo ni pamoja na kuongeza kasi ya kusikiliza mashauri mahakamani ambapo kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Repoa, hatua hiyo ya Mahakama imesaidia   kuongezeka kwa kiwango cha wananchi kuridhishwa na mfumo wa utoaji haki kutoka asilimia 57 mwaka 2015 na kufikia asilimia 72 mwaka 2019.

Maboresho mengine yaliyofanywa na Mahakama ni kusogeza zake karibu zaidi na wananchi kwa kujenga majengo mapya na kukarabati yaliyochakaa, kuanzisha huduma ya Mahakama inayotembea (Mobile Court), kuboresha sheria na kanuni mbalimbali na kutumia teknolojia ya habari na Mawasiliano katika kurahisisha shughuli za utoaji haki ikiwemo matumizi ya ‘Video Conference’.

Aidha, kiwango cha kuridhika kwa wateja kutokana na huduma zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania kimeongezeka kutoka asilimia 61 mwaka 2015 na kufikia asilimia 78 mwaka 2019. Aidha, wananchi waliohojiwa na kukiri kutolipia baadhi ya nyaraka za kimahakama imeongezeka kutoka asilimia 38 mwaka 2015 na kufikia asilimia 71 mwaka 2019.

Katika kipindi hicho cha miaka mitano, Mahakama imefanikiwa kuondoa mlundikano wa mashauri yenye muda mrefu mahakamani (Case backlog) kutoka asilimia 12 kati ya mashauri 96,852 yaliyobaki Desemba 2015 na kufikia asilimia 5 kati ya mashauri 3,805 yaliyobaki Desemba 2019.

Mahakama pia imefanikiwa kumaliza mashauri yenye migogoro ya kibisashara na uchumi. Hadi kufikia Desemba 2019, mashauri yanayobishaniwa kodi ya kiasi cha shilingi bilioni 47 na mashauri 89 ya Uhujumu uchumi yenye thamini ya shilingi bilioni 44 yalimalizika katika ngazi ya mahakama ya Rufani.

Wajumbe kutoka Benki ya Dunia walifika nchini kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama unaotekelezwa na Mahakama ya Tanzania.

Comments (0)

Leave a Comment