Post Details

WAJUMBE WA BENKI YA DUNIA WATEMBELEA MAHAKAMA KUU KIGOMA

Published By:LYDIA CHURI

Wajumbe kutoka Benki ya Dunia wamekagua jengo jipya la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma ili kuona ufanisi wa mfumo wa haki Jumuishi (intergrated Justice center) ambapo wamepongeza namna Mahakama hiyo ilivyojipambanua kuwahudumia wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua jengo hilo, Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia Bwn. Walid Malik amesema kufuatia hatua hiyo nzuri ya Mahakama Kuu ya Kigoma wananchi sasa wataanza kufika Mahakamani hapo kujifunza namna huduma inavyotolewa.  

Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Watumishi wa Mahakama na wajumbe wa Benki ya Dunia, Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya kigoma Mhe. Ilvin Mugeta alisema jengo hilo limeanza kutoa huduma rasmi Disemba 10, mwaka jana ambapo alisema ushirikiano wa wadau waliopo katika Jengo hilo pamoja na mikakati waliyojiwekea vimechangia kusukuma mashauri ya madai na jinai kumalizika kwa wakati. 

Kwa upande wake, Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mheshimiwa Arnold Kirekiano alieleza kuwa asilimia themanini na tano (85%) ya mashauri yaliyomalizika hadi January 31, 2020 yalishughulikuwa ndani ya miezi minne, jambo  lililopelekea kanda hiyo kuweka mkakati wa kupunguza muda wa mashauri mahakamani.

Naye Mwenyekiti wa Mawakili Mkoa wa kigoma Bw. Ignatus Kagashe ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kujenga jengo hilo ambalo ni wezeshi kimiundombinu na linalotoa fursa za ofisi kwa wadau mbalimbali.

Alisema uanzishwaji wa Mahakama Kuu kanda ya kigoma umewapunguzia gharama wananchi wa Mkoa wa Kigoma ambao awali walikuwa wakipata huduma za Mahakama Kuu Mkoani Tabora.

Wajumbe kutoka Benki ya Dunia wamewasili nchini kwa ajili ya kufanya tathmini ya maboresho yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa majengo ya Mahakama.

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment