Post Details

TAMISEMI YAOMBWA KUTENGA FEDHA KWA AJILI YA KAMATI ZA MAADILI

Published By:LYDIA CHURI

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ameiomba ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutenga bajeti kwa ajili ya kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama za Mikoa na wilaya ili ziweze kutekeleza majukumu yake kama sheria inavyozitaka ikiwa ni pamoja na kukutana na kuwasilisha taarifa zake kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya kutotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria kutokana na upungufu wa bajeti.  Kamati hizi ziliundwa baada ya kutungwa kwa sheria ya Usimamizi wa Mahakama namba 4 ya mwaka 2011.

Akizindua Mwongozo wa Uendeshaji wa kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama leo jijini Dodoma, Waziri Mahiga amesema Serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria itahakikisha Tume ya Utumishi wa Mahakama inapatiwa rasilimali fedha  kwa ajili ya kuendesha shughuli zake ikiwemo Kamati za Maadili za  Maafisa wa Mahakama kwa ufanisi unaotakiwa.

Amewataka wajumbe wa kamati hizo kuutumia mwongozo huo wa uendeshaji kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwepo kwani matarajio ya Tume na Serikali ni kuona utekelezaji wa majukumu unaozingatia matakwa ya sheria, kanuni na taratibu.

Alisema kwa kuona umuhimu wa kuimarisha dhana ya utawala bora kupitia sheria ya uendeshaji wa Mahakama, Serikali imeruhusu uwepo wa kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama ambazo ni pamoja na; Kamati ya Maadili ya Majaji, Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama na Kamati ya Maadili ya Mahakama ya Mkoa na wilaya.

Kwa mujibu wa Waziri Mahiga, kamati hizi zina nafasi kubwa katika kusimamia, kuendeleza na kudumisha maadili ya Utumishi wa Mahakama. Aliongeza kuwa suala la kuwapatia wajumbe wa kamati Mwongozo huo ni suala la msingi kwani sasa watatekeleza majukumu yao kwa kufuata msingi wa sheria, kanuni  na taratibu.

Akizungumzia Maadili kwa watumishi wa Mahakama, Waziri Mahiga amewataka watumishi wachache  wanaoendelea na vitendo vya ukiukaji wa maadili kuacha mara moja ili kulinda heshima ya Mhimili wa Mahakama na pia kwa usalama wa ajira zao.

Aidha amesema wananchi wengi bado hawafahamu uwepo wa kamati za maadili na majukumu yake ambapo wamekuwa wakipeleka malalamiko yao dhidi ya Maafisa wa Mahakama kwenye Mamlaka zisizo sahihi na hivyo kupoteza muda mwingi.

Ameitaka Tume ya Utumishi wa Mahakama kutoa Elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya uendeshaji wa Kamati za Maadili na huduma zinazotolewa na kamati hizo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza kwa niaba ya wakuu wote wa mikoa nchini amesema kupitia Mwongozo uliozinduliwa, Serikali imeruhusu uwepo wa wa sura ya utendaji wa pamoja baina ya mihimili yote mitatu ya dola.

Alisema palipo na Maadili pana amani, haki, uaminifu katika utendaji kazi, umoja na ushirikiano. Aliongeza kuwa kuwepo kwa maadili pia ni ni kichocheo cha Maendeleo ya Taifa.

Aidha Dkt. Nchimbi alisema suala la uwepo wa Maadili miongoni mwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania husaidia kuifanya Mahakama kuwa rafiki na karibu zaidi na wananchi.  

Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya huongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao hupokea na kuchunguza malalamiko dhidi Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za wilaya na Mahakama za Mwanzo.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment