Post Details

JAJI KIONGOZI AZINDUA JENGO LA MAHAKAMA YA MWANZO IGUGUNO

Published By:LYDIA CHURI

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt.Eliezer Mbuki Feleshi amezindua jengo la Mahakama ya Mwanzo Iguguno na kuwataka watumishi wa Mahakama hiyo kuwa na maadili mema kwa kupingana na vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Iguguno, Jaji Kiongozi amesema Mahakama ya Tanzania ni Taasisi hivyo haiwezi kujishirikisha na vitendo vya rushwa bali anayeshiriki vitendo hivyo ni mtu binafsi.

Amesema Mahakama inavyo vyombo vya kisheria vya kushughulikia maadili ikiwemo kamati ya Maadili ya Majaji na Kamati ya maadili ya Maafisa wa Mahakama.

Aidha, Dkt. Feleshi ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa wilaya nchini kuongeza kasi  katika kufuatilia malalamiko yanayotolewa dhidi ya Watumishi wa Mahakama wakiwemo Mahakimu na kuchukua hatua stahiki pale wanapokuwa na ushahidi wa kutosha.

“Watumishi wa Mahakama na wananchi kwa ujumla tubadilike kwani haki hainunuliwi wala haiuzwi”, alisema Jaji Kiongozi.

Kuhusu kuanzishwa kwa masjala ndogo ya Mahakama ya wilaya ya Mkalama ndani ya jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Iguguno, Jaji Kiongozi amesema masjala hiyo inaweza kuanzishwa endapo wadau wanaofanya kazi na Mahakama wataridhia. Baadhi ya wadau hao ni Polisi, Magereza, Takukuru, Mkemia Mkuu wa Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali.

Akizungumzia mashauri ya Mirathi, Dkt. Feleshi amesema Mahakama ina changamoto na mashauri hayo kwa kuwa huchukua muda mrefu kumalizika kutokana na familia husika kuchelewesha au kutochagua msimamizi wa mirathi mapema.

Kuhusu usikilizwaji wa mashauri, Jaji Kiongozi amewataka Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo Iguguno kumaliza mashauri kwa wakati kwani Mahakama ya Tanzania inapenda kuona mashauri yaliyofunguliwa yanaisha siku hiyo hiyo na hili litawezekana endapo wanachi watafika mahakamani na mashahidi.  

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani aliwata watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Iguguno kufanya kazi kwa kufuata maadili mema.

Jengo la Mahakama ya Mwanzo Iguguno lilianza kujengwa na wananchi na baadaye mradi huo kuchukuliwa na Mahakama ya Tanzania na kukamilika mwaka 2018 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 115.    

  

 

Comments (0)

Leave a Comment