Post Details

RAIS MAGUFULI AFURAHISHWA NA MABORESHO YA MAHAKAMA

Published By:Mary C. Gwera

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utendaji mzuri wa kazi ikiwemo matumizi  bora ya fedha za Serikali.

Akizungumza katika sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini, Februari 06, 2020 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwl. Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais alionyeshwa kufurahishwa na utendaji wa Mahakama katika Maboresho yaliyofanyika ikiwemo kupunguza mlundikano na ucheleweshaji wa mashauri, matumizi ya Tehama, Huduma ya Mahakama inayotembea ‘mobile court services’, maboresho ya miundombinu ya majengo na kadhalika.

“Leo nina furaha kubwa sana, kwa kuwa Mahakama imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka minne (4) iliyopita, hivyo nakupongeza Mhe. Jaji Mkuu na Watumishi wote wa Mahakama kwa kazi nzuri ya utoaji haki nchini,” alisema Mhe. Rais.

Mbali na pongezi hizo, Mhe. Rais aliisifu pia Mahakama kwa matumizi mazuri ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Mhimili huo.

“Hakuna ufisadi Mahakama, fedha zinazotolewa zinatumika vizuri, hivyo nawapongeza sana,” alieleza Mhe. Dkt. Magufuli.

Aidha; Mhe. Rais aliongeza kuwa suala la ucheleweshwaji wa usikilizwaji wa Mashauri limepungua kwa asilimia 100, huku akitoa mfano kuwa katika mwaka 2016 mlundikano wa mashauri umepungua kutoka asilimia 12 hadi asilimia 5 kwa sasa.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alizungumzia juu ya mafanikio ya uanzishwaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama ‘Mahakama ya Mafisadi’ kuwa Mahakama hiyo imepata mafanikio makubwa.

“Tangu Mahakama ya Mafisadi ianzishwe mwaka 2016 jumla ya mashauri ya uhujumu uchumi 119 yamesajiliwa na mashauri 89 yamemalizika ambapo faini ya sh. bil. 13.6 na fidia ya bil.30.6 zimetolewa,” alieleza.

Aliongeza kuwa uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi umeondoa dhana iliyokuwa imejengeka miongoni mwa wananchi kuwa mapambano dhidi ya rushwa nchini yamekuwa yakiwalenga wananchi wa chini na kuwaacha vigogo.

Hali kadhalika Mhe. Rais amemuhakikishia Mhe. Jaji Mkuu kushughulikia changamoto zilizopo ndani ya Mahakama ikiwemo upungufu wa rasilimali watu, maslahi duni ya watumishi, pamoja na kuongeza fedha matumizi ‘OC’.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mhe. Rais, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema Mfumo wa Kielekitroniki wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (JSDS II) uliouzindua mwaka jana umeendelea kuwa msaada mkubwa katika kurahisisha shughuli za uendeshaji wa mashauri.

Mhe. Prof. Juma alisema kuwa mfumo huu ambao unatoa taarifa kwa wadau kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi na barua pepe, umeunganishwa pia na wa malipo ya serikali (Government Electronic Payment Gateway (GEPG)) na Mfumo wa Kusimamia Mawakili (TAMS).

“Kuunganishwa Mfumo wa JSDS2 na mfumo wa malipo ya Serikali umeiwezesha Mahakama kudhibiti ukusanyaji wa Tozo na Ada. Udhibiti huu umewezesha ongezeko la maduhuli toka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2017 mpaka shilingi bilioni 2.5,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka jana jumla ya mashauri 2,435 yalifunguliwa kwa kielektroniki. Lengo la Mahakama ni kuendelea kuboresha mfumo kwa kutumia wataalamu wa ndani.

Siku ya Sheria nchini, ilitanguliwa na Maonesho ya Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria ambayo kitaifa ilifanyika kuanzia Januari 31 hadi Februari 05 mwaka huu ambapo kwa mwaka huu Kaulimbiu ni “Uwekezaji na biashara; Wajibu wa Mahakama na wadau katika kukuza uwekezaji na biashara.”

Comments (0)

Leave a Comment