Post Details

VIONGOZI WAPYA WA SERIKALI, MAHAKAMA, MAGEREZA WATAKIWA KUWAJIBIKA

Published By:Mary C. Gwera

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Viongozi mbalimbali aliowaapisha kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao mapya waliyopangiwa.

Mapema Februari 03, mwaka huu, Mhe. Rais amewaapisha Viongozi mbalimbali wa Wizara, Mahakama, Majeshi na Mikoa aliowateua mwishoni mwa wiki kushika nyadhifa mbalimbali katika hafla fupi ya uapisho iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Nendeni mkaijenge Tanzania kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla, hivyo ni wajibu wenu kutekeleza majukumu yenu huku mkimtanguliza Mungu,” alisema Mhe. Rais.

Mhe. Rais aliongeza kuwa hana shaka na Viongozi aliowateua huku akitoa sifa za kila mmoja wao na kuwataka kutekeleza majukumu yao wakijua kuwa wanafahamika.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais kwa uteuzi wa Viongozi waandamizi wa Mahakama kwani itasaidia kurahisisha utendaji kazi.

“Mhe. Rais nikushukuru kwa dhati juu ya uteuzi wa Viongozi wa Mahakama uliotupatia, kwa kuwa ni sehemu muhimu katika utendaji kazi wa Mahakama, hususani upatikanaji wa Msajili Mkuu ambaye ndiye injini ya shughuli za Mahakama, Mkuu wa Wasajili na Mahakimu wote na vilevile kiungo kati ya Mahakama na Serikali,” alieleza Mhe. Jaji Prof. Juma.

Vilevile Mhe. Jaji Mkuu alimshukuru pia Mhe. Rais kwa uteuzi wa Makamishna watatu (3) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, kwa kuwa Tume hiyo pia ina wajibu mkubwa kwa ustawi wa Mahakama.

Mbali na kumshukuru Mhe. Rais kwa uteuzi wa Viongozi wa Mahakama na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Jaji Mkuu aliwapongeza Viongozi wote walioapishwa huku akionyesha kufurahishwa pia na uteuzi wa Kamishna Jenerali wa Magereza kwa kuwa ni mdau muhimu wa Mahakama.

Viongozi walioapishwa katika hafla hiyo ni Makatibu Wakuu watano, Msajili Mkuu wa Mahakama, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Naibu Katibu Mkuu, Makatibu Tawala wa mikoa mitatu, Kamishna Generali wa Magereza na Kamishna Jenerali wa Zima-moto na Uokoaji.

Aidha, katika hafla hiyo; Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alimuapisha Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Shamira Sarwatt.

Comments (0)

Leave a Comment