Post Details

WATUHUMIWA 60 WA UTUPAJI TAKA NGUMU OVYO WAFIKISHWA MAHAKAMA INAYOTEMBEA

Published By:Mary C. Gwera

Mahakama Inayotembea leo imeendesha mashauri katika ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine maarufu ‘ Mahakama ya Jiji’ kwa ajili ya kusikiliza mashauri mbalimbali ya watuhumiwa wapatao 60, wa kosa la utupaji taka ngumu ovyo   baada ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam kufanya operesheni maalum.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mratibu wa Mahakama hiyo, ambaye pia ni Hakimu Mkazi, Mhe. Moses Ndelwa alisema watuhumiwa hao, wamekamatwa baada ya kupatikana na kosa la kuvunja Sheria ya Mazingira namba mbili ya Mwaka 2004, pamoja na sheria ndogondogo za jiji.

‘Tuko tayari tumejipanga vizuri kwa ajili ya kusikiliza mashauri haya, ambapo tumeandaa hati zao za mashtaka leo, yanasikilizwa leo na kutolewa hukumu leoleo,’ alisema Ndelwa.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa akikiri kosa anatozwa faini ya kuanzia sh, 20,000/= na isiyozidi sh. 300,000/= kulingana na kosa, au kifungo kisichozidi miezi sita jela.

Mashauri hayo yameendeshwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Sokoine, Mhe. Anipha Mwingira, ambapo alisema kwa kundi la kwanza la watuhumiwa hao 16, kati yao 13 wamekiri kosa na wamekubali kulipa Sh. 20,000 kila mmoja, hawakukubali na mmoja hakufika mahakamani hapo.

Watuhumiwa hao, walikamatwa baada ya Manispaa ya Ilala kuendesha operesheni maalum, akizungumzia kuhusu suala hilo. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bi. Sophia Mjema alisema zoezi hili itakuwa ni endelevu. Pia watuhumiwa hao walikamatwa kwa makosa ya kutupa ovyo taka ngumu mfano maganda ya pipi na chupa za maji ya kunywa.

Hivyo aliwataka wakazi wa eneo hilo kuacha tabia ya utupaji taka ovyo, badala yake watupe sehemu husika na kama hakuna waziweke mpaka watakapo pata mahali maalum pa kutupa ili kuepuka kufikishwa mahakamani.

‘Hii ni mara ya kwanza kwa Manispaa ya Ilala kufanya operesheni hii, na mashauri kuendeshwa kwa kutumia mahakama hii. Pia tuna mpango wa kufanya operesheni nyingine kwa ombaomba na anayempatia fedha ombaomba kwa kushirikiana jiji nzima, kwa kuwa tunataka kila mtu afanye kazi kama Mhe. Rais Dkt. John Magufuli anavyoelekeza,’ alisema Mjema.

Aliongeza kuwa ikiwa mtu anataka kutoa msaada aende katika vituo vya watoto yatima, kanisani au msikitini na si kutoa barabarani.

Hii ni mara ya pili kwa Mahakama Inayotembea kuendesha mashauri kupitia operesheni maalum, mara ya kwanza ilifanyika katika viwanja wa Biafra, Kinondoni, ambapo jumla ya watuhumiwa 100 walikamatwa kwa kosa la kutiririsha maji taka, katika mashauri 28.

Kwa mujibu wa Mhe. Ndelwa alisema watuhumiwa hao, wengi walilipa faini isiyozidi Sh. 80,000/=.

Comments (0)

Leave a Comment