Post Details

JAJI MKUU: UJENZI WA MAHAKAMA NI JUKUMU LA MIHIMILI YOTE

Published By:Mary C. Gwera

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema mihimili yote mitatu ya Dola inao wajibu wa kuhakikisha huduma za utoaji haki zinapatikana nchini hususani kwenye wilaya zote 139.

Akizindua rasmi jengo la Mahakama ya wilaya ya Kilwa leo wilayani humo, Jaji Mkuu amesema ujenzi wa jengo hilo la Mahakama ni kielelezo cha ushirikiano kati ya Mahakama na mihimili ya Serikali na Bunge katika kuiwezesha Mahakama na mihimili ya Serikali na Bunge katika kuiwezesha Mahakama kuwapelekea wananchi huduma.

Akizungumzia wilaya zenye huduma za Mahakama za wilaya, Prof. Juma alisema ni wilaya 111 kati ya 139 ndizo zenye huduma za Mahakama za Wilaya huku wilaya 28 zikiwa bado zinahudumiwa na Mahakama za Wilaya zilizo jirani. Alifafanua kuwa wilaya zilizosalia zinatumia majengo aidha ya kupanga au kuazimwa na Taasisi nyingine za Serikali.

“Safari ya kufikia azma ya kila wilaya kuwa na jengo la kisasa la Mahakama bado ni ndefu” alisema Jaji Mkuu huku akiwataka wananchi wa Mahakama pamoja na wananchi wa wilaya ya Kilwa kulitunza jengo hilo jipya ili lidumu kwa muda mrefu.

Alisema kukamilika kwa jengo hilo la kisasa la Mahakama ya wilaya ya Kilwa ni hatua muhimu ya kusogeza huduma za kimahakama karibu zaidi na wananchi na pia kuharakisha shughuli za utoaji wa haki kwa wananchi wa Kilwa.

Alisema shughuli za Mahakama katika majengo mapya yanayojengwa hivi sasa na Mahakama zitatumia mifumo ya TEHAMA baada ya kuunganishwa na mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Aliongeza kuwa ili kutatua changamoto ya uhaba na uchakavu wa majengo. Mahakama imeandaa Mpango wa miaka mitano (5) wa Maendeleo ya Miundombinu (2016/17-2020/21).

Alitoa rai kwa wananchi kuwa Mahakama ni kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo watumishi wa Mahakama wanaotoa huduma wanastahili heshima kutoka kwa wananchi kama ambavyo wananchi wanastahili heshima na huduma bora kutoka kwa watumishi.

Kuhusu mashauri, Jaji Mkuu aliwataka wananchi kutofungua mashauri mahakamani kwa lengo la kukomoana au kupoteza muda bali watumie Mahakama kama chombo cha kupata haki wanayostahili na watambue kuwa wanapofungua shauri Mahakamani wasifikirie kuwa ni lazima washinde hata pale ambapo hakuna ushahidi wa kutosha kushinda kwani shauri hujengwa na ushahidi na si hisia au tuhuma peke yake.

Awali akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kilwa, Mtendaji Mkuu wa Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru amewaasa wananchi kuwa na utashi wa kujifunza sheria ili waziheshimu na kuwataka watumishi wa Mahakama kuendelea kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kila wiki.

Amewataka wananchi na watumishi wa Mahakama kulitunza jengo lililozinduliwa ili liweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu zaidi.

Jengo la Mahakama ya wilaya ya Kilwa linalojumuisha Mahakama ya Mwanzo nay a wilaya limejengwa kwa kutumia teknolojia ya Moladi na Kampuni ya Moladi Tanzania na kusimamiwa na Chuo Kikuu cha Ardhi. Jengo hili limegharimu kiasi cha shilingi 705,106,540/-.

Comments (0)

Leave a Comment