Post Details

MAFUNZO HUDUMA KWA MTEJA MUHIMU KUBORESHA UTENDAJI KAZI; JAJI MARUMA

Published By:Mary C. Gwera

Na Dhillon John, Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma  ameagiza Watendaji wa Kituo hicho kuandaa Mafunzo ya Huduma kwa mteja  mara nyingi iwezekanavyo lengo likiwa ni kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi wanaowahudumia.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akifungua Mafunzo ya siku moja ya Huduma kwa Mteja yaliyofanyika katika Ofisi za Kituo hicho jijini Dar es Salaam, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma alisema Mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanasaidia kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi.

“Mafunzo haya ni muhimu sana na yalikuwa yanasubiriwa kwa muda mrefu, hivyo ni rai yangu kuwa mafunzo haya yawe yanatolewa mara kwa mara hata kila baa ya miezi sita ili kukuza utoaji wa huduma kwa mteja,” alisema Mhe. Maruma.

 Akiwasilisha mada hiyo kwa Watumishi wa Kituo hicho, Mwezeshaji wa Mafunzo, Bw. Remigius Kyaruzi alisema kuwa, utoaji wa huduma kwa mteja ni njia mojawapo ya kujitangaza hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kufanya jitihada za kubadili mtazamo na kuwa na mtazamo chanya ili kuweza kuwahudumia wateja kwa namna bora zaidi.

Mkufunzi huyo ambaye pia ni Mtumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke aliongeza kuwa, ni muhimu pia kwa Taasisi kuangalia mbinu mpya za kujitangaza (Organization branding) ili huduma inayotolewa kwa wateja iweze Kwenda sambasamba na uboreshaji wa huduma.

Alizitaja njia za kuhudumia wateja ni kwa njia ya ana kwa ana, kwa njia ya mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii (social media) pamoja na njia ya barua pepe.

Kwa upande wake, Jaji wa Kituo hicho, Mhe. Dkt. Zainab Mango alisema kuwa, ili Kituo kiwe kizuri ni muhimu kila Mtumishi kukubali kujifunza na anapokosea inapaswa aambiwe ukweli ili kutorudia kosa na hatimaye kupata matokeo chanya.

Watumishi wa Kituo hicho kwa pamoja waliahidi kubadilika katika utoaji wa huduma ili Kituo hicho kiwe mfano wa Taasisi katika utoaji huduma nzuri kwa wateja wanaowahudumia.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Mhe. Jaji Dkt. Mango, Jaji wa kituo hicho, Mhe. Wanjah Hamza, Naibu Msajili Mfawidhi wa Kituo hicho, Mtendaji, Bi. Hellen Mkumbwa pamoja na Watumishi wote wa Kituo hicho.

Comments (0)

Leave a Comment