Post Details

UTEUZI WENU UNATARAJIWA KUONGEZA UFANISI NA UBORA WA MAAMUZI KWA WAKATI: JAJI KIONGOZI

Published By:kansha.innocent

Na Innocent Kansha – Mahakama, Lushoto

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewambia Majaji Wapya waliomaliza mafunzo elekezi ya utayari kuwa uteuzi wao umebeba matarajio kwa Umma, mamlaka ya uteuzi na Mahakama ya Tanzania. 

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo elekezi ya namna bora utendaji kazi wa Majaji leo tarehe 16 Septemba, 2022 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto yaliyodumu kwa muda wa wiki tatu, Mhe. Siyani alisema, kwa upande wa eneo la usikizaji wa mashauri ujio wao unatarajiwa kushusha mzigo kazi (workload) kwa kila Jaji. Mtakumbuka kabla ya kuteuliwa kwenu kila Jaji alikuwa na wastani wa mashauri 340 kwa mwaka, kufuatia kuteuliwa na kuapishwa kwenu, idadi hiyo ilishuka mpaka wastani wa mashauri 265.

Kushuka kwa idadi hiyo ya mashauri ambayo kila Jaji anapaswa kuwa nayo ni nafuu kwa Majaji, lakini nini Mahakama na watanzania wanatarajia kuhusu ujio wenu. Wananchi wanasubiri kuona kasi ya usikilizwaji wa mashauri na utoaji wa maamuzi kwa wakati ukiongezeka, wanataraji kuona ufanisi na ubora wa maamuzi ukiongezeka.

“Hata hivyo, kwa sasa na hasa baada ya majaji 3 kustaafu mmoja mwezi uliopita na wawili mwezi Septemba, mzigo kazi kwa kila Jaji umeongezeka kufikia wastani wa mashauri 275 kwa mwaka, kulingana na hali ya Kituo, hiki ndicho kiasi cha chini cha mashauri ambayo mnapaswa kukitarajia mtakapokwenda kwenye vituo vyenu. Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na wastani wa mashauri 411 ambayo kila Jaji alikuwa nayo mwaka 2021”, alisema Jaji Kiongozi.

Kwa hiyo mtaona, hata kabla ya uteuzi wenu idadi ya wastani wa mashauri ambayo kila Jaji alipaswa kuwa nayo kwa mwaka, ilipungua. Tafsiri pekee ya kupungua kwa mzigo kazi kabla ya uteuzi wenu, ni kuwa kazi kubwa ilifanywa na Majaji wenzenu.

Kuhusu mlundikano wa mashauri Jaji Kiongozi akasema, kufikia Juni 2022, Mahakama Kuu ya Tanzania, ilikuwa na jumla ya mashauri ya mlundikano, 1433 ambayo ni wastani wa asilimia 10 ya mashauri yote 14,719 yaliyokuwepo kwenye masjala zote za Mahakama Kuu. Mahakama imejiwekea mkakati kuhakikisha inaondokana na mashauri haya ya muda mrefu.

“Kila Kanda na Divisheni ya Mahakama Kuu, ina mkakati wake wa kupambana na mashauri haya. Mtakapokwenda kwenye vituo vyenu hakikisheni mnashiriki utekelezaji wa mikakati hiyo kwa pamoja na mambo mengine; kuyapa kipaumbele mashauri ya mlundikano na kuzuia mashauri mapya yasipevuke na kuwa mlundikano. Kwa kufanya hivyo pekee mtatimiza dira ya Mahakama ya kutoa haki kwa wakati na kujenga imani ya wananchi kwa Taasisi yetu”, alisisitiza Jaji Kiongozi kwa Majaji hao.

Jaji Siyani akawakumbusha Majaji kuwa, ni vyema wakafahamu kuwa mfumo uliorithiwa kutoka kwa wakoloni, umewafanya Majaji kuwa wasikilizaji zaidi na umechangia kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa mashauri na hivyo kusababisha mlundikano. Kwa hiyo zama za Majaji kuwaachia wadaawa kuiongoza Mahakama na Majaji kubaki kama wasikilizaji, ni zama zilizopitwa na wakati.

Aidha, Jaji Kiongozi aliwapongeza Majaji wote kwa kuonyesha juhudi kubwa, nidhamu ya hali ya juu na kwa kutambua kuwa watatumia elimu kubwa waliyoipata ili iwasaidie kuwatumikia vema wananchi katika vituo vyao vya kazi.

Comments (0)

Leave a Comment