Post Details

MAHAKAMA YAPONGEZWA KWA MATUMIZI MAZURI YA FEDHA

Published By:LYDIA CHURI

Na Waandishi- Mahakama Ruangwa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa matumizi mazuri ya fedha katika ujenzi wa majengo yake.

Akizindua rasmi jengo jipya la Mahakama ya wilaya ya Ruangwa leo, Waziri Mkuu amesema hatua ya Mahakama kutumia ujenzi gharama nafuu katika ujenzi wa jengo hilo ni matumizi mazuri ya fedha za Umma.

“Mahakama ya Tanzania ni chombo ambacho kimemuunga mkono Rais wetu ambaye amekuwa akisisitiza matumizi mazuri ya fedha za Umma, hivyo nampongeza sana Jaji Mkuu wa Tanzania”, alisema Waziri Mkuu.  

Jengo hilo linalojumuisha ngazi mbili za Mahakama ambazo ni Mahakama ya Mwanzo na ya wilaya ya Ruangwa limegharimu kiasi cha shilingi milioni 782,547,340, ambayo ni ndogo ukilinganisha na Wazabuni wengine waliotaka kujenga jengo hilo kwa zaidi ya shilingi bilioni moja.

Waziri Mkuu amewataka watumishi wa Mahakama kuendelea kutoa haki kwa wote kwa kuwa ni Mhimili muhimu wa dola ambao huchangia katika kuleta amani ya nchi.

Amemshukuru Jaji Mkuu kwa kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi wa Ruangwa kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama kubwa walizokuwa wakiingia wananchi kwa kusafiri umbali wa takribani kilometa 180 kufuata huduma za Mahakama mkoani Lindi.

“Wananchi wa wilaya ya Ruangwa mmepata bahati ya kupata jengo hili zuri, hivyo nawahimiza kutunza na kulinda miundombinu yake bila kufanya uharibifu wa aina yoyote”, alisisitiza.  

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama kutoa huduma bora zinazoendana na uzuri wa jengo na kuachana na tabia na mienendo inayoenda kinyume na maadili.

“Tukumbuke kuwa Mahakama ni mali ya wananchi na wanayo haki ya kupatiwa huduma bora hivyo tutoe huduma itakayowaridhisha wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki”, alisema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu pia amewaasa wananchi kutumia Mahakama kutatua migogoro yao badala ya kuegesha kesi mahakamani. Amesema wananchi pia wanayo haki kisheria ya kutumia usuluhishi kabla ya kufungua mashauri  mahakamani.   

Aidha amewaasa wananchi na watumishi wa Mahakama kutunza miundombinu ya jengo hilo ili lidumu kwa muda mrefu kwa kuwa mahakama bado ina safari ndefu katika kujenga majengo yake.

Jaji Mkuu pia ameiomba Serikali kuanzisha Mahakama mahali yanapoanzishwa maeneo ya utawala. Lengo la Mahakama ni kufikisha huduma ya utoaji haki kwa kuwa na majengo yake katika kila kata, tarafa, wilaya na Mikoa.

 

Comments (0)

Leave a Comment