Post Details

MAJAJI WA MAHAKAMA KUU WASHUHUDIA MAAJABU YA MAPANGO YA AMBONI

Published By:faustine.kapama

Na. Ibrahim Mdachi, IJA - Lushoto

Majaji 26, wakiwemo wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar wakiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt Paul Kihwelo wametembelea Mapango ya Amboni mkoani Tanga hivi karibuni kujionea maajabu yaliyomo sambamba na kusikiliza hekaya za kusisimu kuhusu mapango hayo.

Akitoa maelezo mafupi katika ziara hiyo, mmoja wa Waongoza Watalii aliwafahamisha Majaji hao kuwa mapango hayo yanayoundwa na miamba chokaa yaliyoko katika eneo linalopitiwa na mito ya asili yenye ukubwa wa takriban eneo la kilomita za mraba 234 yanaaminika kuwa chini ya usawa wa bahari miaka milioni 20 iliyopita.

Alisema Pango hilo lenye moja ya lango linavutia lenye umbo la bara la afrika linaaminika kuwa ni eneo pekee na la kihistoria linakutanisha imani za uislamu, ukristo sambamba na imani za kijadi katika eneo moja kutokana na uwepo wa alama mbalimbali zilizomo katika mapango hayo.

Majaji hao walipata fursa ya kujionea eneo lenye maandishi ya lugha za kiarabu yanayotaja jina la mwenyezi mungu na eneo lenye mfanano wa kanisa lenye kiti cha mwongozaji ibada.

Kwa upande wa dini za kijadi, Majaji walipita katika eneo maarufu linalojulikana kwa jina la “Mzimu wa Mabavu” ambalo limekuwa likiwakutanisha watu kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa matambiko ya mizimu ambapo hapo awali yalikuwa yakitumiwa na watu wa makabila yaliyoishi jirani na eneo hilo wakiwemo Wasambaa, Wadigo, Wabondei na Wasegeju tangu Karne ya 16. Iliaminika kuwa miongoni mwa mengi yanayoweza kufanywa na mizimu hiyo ni pamoja na kutatua matatizo ya uzazi, kuongeza kipato na kutib au kuponya magonjwa mbalimbali.

Majaji hao walielezwa kuwa mapango hayo yanaaminika kuwa na njia za chini kwa chini zinazosemekana kutokea mkoani Kilimanjaro na Mji wa Mombasa nchini Kenya sambamba na simulizi za kupotea kwa watalii wawili wa kizungu walioonekana kuingia mapangoni humo na mbwa wao mnamo mwaka 1941 na miaka kadhaa baadaye mbwa wao kuonekana kando ya Mlima Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro.

Mwongoza Watalii huyo aliwaeleza Majaji pia kuwa mapango hayo yalitumiwa katika harakati za kuwapinga walowezi  mkoani Tanga ambapo mnamo mwaka 1922 kupitia hekaya maarufu iliyowahusu wanaharakati wawili waliofahamika kwa majina ya Paulo Hamisi na Samuel Otango ambao ni raia wa Tanganyika na Kenya ambapo watu hawa waliwahi kutumia kituo namba tatu ndani ya pango kubwa kama maficho kati ya mwaka 1952 na 1956,  chumba chembembe chenye urefu kwenda juu katika harakati zao dhidi ya walowezi wa kikoloni na kuwawia ugumu wanausalama wa kikoloni kuwakamata.

Majaji walipata fursa ya kuingia kwenye chumba hicho chembamba ambapo iliwalazimu kuingia kwa kuinama kwa taabu kukifikia chumba hicho. Miongoni mwa maeneo mengine yaliyosisimua nyoyo za Majaji ni pamoja na njia nyembamba sana yenye kiza totoro ambapo baadhi yao walionyesha uthubutu na kufanikiwa kupita katika eneo hilo.

Aidha, Majaji walipata fursa ya kuona maumbo ya viumbe yaliyotoka na mabadiliko ya kikemikali ya miamba hiyo (miamba chokaa) na kuunda taswira hizo ikiwemo wanyama kama Mamba, Tembo, Mijusi, mwewe aliyebeba samaki na alama nyingine ni pamoja na sanamu ya bikira maria, bao la kete, theluji juu ya mlima Kilimanjaro, bawa la kuku na unyayo wa mguu wa binadamu, na mnyama chui inayotokana na mrundikano wa vumbi na udongo ambao hunywea pamoja na maji ya mvua hatimaye kuganda katika paa la pango lililoko umbali wa mita 25.

Mapango hayo ya Amboni yanayopatikana katika eneo la Kiamoni, Kata ya Kiamoni, Tarafa ya Chumbageni, Wilaya ya Tanga umbali wa kilomita 8 toka Tanga mjini kupitia barabara kuu ya inayoelekea Mombasa nchini Kenya, ni eneo zuri la kupumzikia, kwa tafiti za kihistoria, kijiografia, kijiolojia, n.k

Mbali na matumizi hayo, kampuni ya kigeni iliyojulikana kama “Amboni Limited” ilimiliki mashamba ya mkonge katika eneo hili na kuliweka chini ya himaya yake mwaka 1892 ili kulitumia kama sehemu ya kupumzikia kutokana na kuwa na mazingira tulivu, mwaka 1922, miaka 30 baadaye serikali ilitangaza eneo hili kuwa eneo la hifadhi.

Mwaka 1937 ilipitishwa sheria ya mambo ya kale (Monuments Preservation Ordinace of 1937) iliyofuatiwa na ile ya 1953 (Monuments Preservation Ordinace of 1953) ambayo ilitumika kulinda mambo ya kale ikiwa ni pamoja na mapango ya amboni. Mwaka 1963 serikali ya Tanganyika ikayaweka mapango chini ya usimamizi wa idara ya mambo ya kale.

Mwaka 1964 serikali ilisimamisha sheria ya kikoloni ya 1937 na 1953 na kupitisha sheria ya mambo ya kale ya mwaka huo (The Antiquities Act of 1964) iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1979 (Amendments Acts of 1979) kwa ajili ya kulinda mambo ya kale nchini. Kwa upande wa mapango ya Amboni, mbali na mambo mengine sheria inakataza kuandika au kuchora kwenye kuta za mapango.

Comments (0)

Leave a Comment