Post Details

UNODC – GMCP YAWAJENGEA UWEZO MAHAKAMA NA WADAU WA HAKI JINAI

Published By:kansha.innocent

  • Namna ya kukabiliana na makosa yanayofanywa Majini na Baharini  

Na Innocent Kansha - Mahakama

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayopambana na madawa ya kulevya, uhalifu na makosa ya jinai “United Nations on Drugs and Crime” (UNODC) kwa kupitia mradi wa kupambana na makosa yanayofanywa Majini na Baharini Duniani “Global Maritime Crime Programme” (GMCP), leo tarehe 12 Septemba, 2022 imeanza kuendesha mafunzo kwa wadau wa utoaji haki jinai kwa njia ya Mahakama ya mfano “Simulated Trial”.

Mafunzo hayo ya Mahakama ya Mfano yanafanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni (IJC) jijini Dar es salaam kwa kipindi cha siku tano kuanzia tarehe 12 hadi 16 Septemba, 2022 yanalenga kuwajengea uwezo wadau wa utoaji haki jinai kwa namna ya kupambana na makosa yanayotendwa baharini kama vile uharamia, biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu, biashara haramu ya binadamu na biashara ya bidhaa haramu.

Katalogi hiyo ya mafunzo itasaidia kuimarisha mfumo wa uendeshaji mashauri ya aina hiyo kwa upande wa Muhimili wa Mahakama, Waendesha mashtaka na Mawakili namna bora ya uendeshaji wa mashauri na makosa ya aina hiyo

Maeneo mengine yatakayofaidika na programu hiyo ya Mahakama ya mfano ni uchunguzi, uandaaji na uendeshaji wa mashauri na mwenendo wa mashauri mahakamani kwa kupitia makosa yanayofanywa majini na baharini

Mazoezi haya yanalenga kubainisha chagamoto za kiutendaji ikiwemo uandaaji wa mashauri, namna ya upokeaji wa ushahidi mahakamani, namna Mawakili wavyowawakilisha wateja wao mahakamani na mamna ya kuivutia Mahakama itoe ushindi kwa upande mmoja wapo.

Lengo kuu la kufanya Mahakama ya mfano ni kumaliza kisheria tatizo la makosa yanayotendwa majini na baharini kwa kuimarisha mifumo ya mamlaka ya kijinai na kiutendaji katika nchi mbalimbali ili kusikiliza, kuamua na kuendesha mashauri yanayohusiana na makosa ya uharamia, usafirishaji wa madawa ya kulevya na makosa mengineyo kwa ufanisi.

Kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa UNODC GMCP itaendelea kuwajengea uwezo maafisa na vyombo ya usimamizi wa sheria za bahari ili waweze kukusanya ushahidi na kutunza wakati wa operesheni ili ushahidi huo uweze kutumiwa na waendesha mashtaka na maafisa wa Mahakama.

Ushirikiano wa taasisi hizi za utoaji haki jinai zitafikia hatua ya kuendesha mashauri ya makosa hayo kwa weledi na kutoa maamuzi ya haki kwa kudhibiti na kusimamia ipasavyo makosa yote ya aina hiyo. Hatimaye itasaidia kukabidhi na kuwasilisha ushahidi kwa ajili ya kuendesha mashauri na kufikia haki kwa ufanisi. Malengo yake ikiwa ni kuhakikisha makosa haya hayajirudii na hili litafanyika kupitia mafunzo hayo ya kesi ya mfano.

Ili kupata matokeo chanya kupitia mafunzo hayo UNODC GMCP wanashirikiana INTERPOL kutoa elimu ya Mahakama ya mfano na baadhi ya nchi katika ukanda wa bahari ya Hindi na ukanda wa Magharibi yamekwisha fanyika ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Seychelles na Mauritius.

Comments (0)

Leave a Comment