Post Details

MAHAKAMA INAYOTEMBEA YATOA HUDUMA MAALUM-KINONDONI

Published By:Mary C. Gwera

Jumla ya mashauri 100 yameanza kusikilizwa na Mahakama inayotembea ‘mobile court’ katika zoezi maalum linalofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kwa wananchi waliokamatwa kwa kosa la utiririshaji wa maji taka katika wilaya hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Hakimu Mkazi ambaye pia ni Mratibu wa shughuli za Mahakama inayotembea, Mhe. Moses Ndelwa alisema zoezi hilo limeanza rasmi Januari 10 mwaka huu katika Viwanja vya Biafra-Kinondoni jijini Dar es Salaam.

“Lengo la zoezi hili maalum ambalo limeanza rasmi leo (Januari 10, 2020) ni kusikiliza mashauri yanayotokana na ‘operation’ maalum inayofanywa na Wilaya ya Kinondoni kwa watu wanaotiririsha maji taka ambayo yamepangwa kumalizika ndani ya siku moja (1),” alieleza Mhe. Ndelwa.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mahakama hii kufanya zoezi maalum la usikilizaji wa mashauri mbali na mashauri ya kawaida inayosikiliza katika ratiba zake za kawaida kwa maeneo inayotoa huduma katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam.

Aidha, huduma ya Mahakama inayotembea ni endelevu na itakuwa ikitolewa katika mazoezi maalum katika maeneo yenye uhitaji maalum katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza ambapo huduma hiyo inapatikana kwa kuanzia.

Akizungumzia mafanikio ya huduma za Mahakama inayotembea, Hakimu huyo Mkazi alisema hadi kufikia Desemba 2019, Mahakama hiyo tayari imesikiliza jumla ya mashauri 95, huku Mwanza ikiwa imesikiliza jumla ya mashauri 57 na Dar es Salaam 38.

Aliongeza kuwa Mahakama hiyo imefanikiwa kuhudumia jumla ya wananchi wanufaika 516 toka kuanza rasmi kwa huduma hiyo na kuwataka wananchi wenye mashauri mbalimbali kutosita kujitokeza kusajili kesi zao katika Mahakama hii.

Mahakama inayotembea imeanzishwa kwa lengo la kusogeza huduma ya utoaji haki karibu zaidi na wananchi waliopo mbali na huduma za Mahakama.

Comments (0)

Leave a Comment