Post Details

JAJI MKUU AWATAKA WATUMISHI WA MAHAKAMA KUTOA HAKI KWA KILA MTANZANIA

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi, Bukombe-Geita

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amezindua majengo mawili likiwemo jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita pamoja na lile la Mahakama ya wilaya ya Bukombe na kuwataka watumishi wa Mahakama kutoa haki kwa kila mtanzania na kwa wakati unaostahili.

Akizindua majengo hayo mkoani humo, Jaji Mkuu amesema kukamilika kwa majengo hayo ya Mahakama kutaharakisha utoaji wa huduma za Mahakama kwa kuwa majengo ni bora na ya kisasa.

Alisema watumishi wa Mahakama wanalo deni kubwa la kuhakikisha kuwa majengo mazuri yanayozinduliwa yanatumika kutoa haki kwa kila mtanzania na kwa wakati unaostahili”, alisema Jaji Mkuu.

“Bila kubadili tabia za utoaji wa huduma, haimaanishi kwamba, kuwepo kwa majengo na miundombinu bora, basi kutakuwa na upatikanaji wa huduma bora kwa mwananchi”, alisema.

Jaji Mkuu alisema kuzinduliwa kwa majengo hayo ya kisasa kutawarahisishia watumishi kuwapa wananchi kile wanachostahili huku akiwataka kutenda haki ili maana halisi ya kuwa na majengo na miundombinu bora itakapodhihirika.

Akizungumzia Mahakama za Hakimu Mkazi Jaji Mkuu alisema kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara, ni mikoa 18 tu ndiyo yenye majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi. Mikoa 8 bado inatumia majengo ya kupanga na ya muda yaliyoazimwa kutoka taasisi nyingine za Serikali na Halmashauri.

Katika mikoa 18 yenye majengo, mikoa 10 ya Morogoro, Mara, Ruvuma, Mwanza, Lindi, Kigoma, Kilimajaro, Shinyanga na Rukwa ina majengo chakavu, kiasi cha kuhitaji ukarabati ama kujengwa upya miradi mingine inayotekelezwa.

Aidha Jaji Mkuu amewataka Viongozi wa Mahakama Mkoa wa Geita kuhimiza na kusimamia matumizi ya TEHAMA na hasa mfumo ulioboreshwa wa Kielekitroniki wa kuratibu mashauri (JSDS II) kwani vyote hivi vikitumika kikamilifu vitasaidia kumaliza mlundikano wa Mashauri (case backlogs).

Kwa upande wa Mahakama za wilaya. Jaji Mkuu alisema kila wilaya hapa nchini inapaswa kuwa na Mahakama ya wilaya ambapo kuna jumla ya wilaya 139 Tanzania bara lakini wilaya 111 tu ndizo zenye huduma moja kwa moja za Mahakama ya wilaya.

Aliongeza kuwa Wilaya 28 zinahudumiwa na Mahakama za wilaya jirani (Concurrent jurisdiction) kwa kutembelewa na Mahakimu huku akitolea mfano wa wilaya ya Geita inayohudumiwa na wilaya ya Nyang’hwale na Mahakama ya wilaya ya Mbogwe inahudumiwa na Mahakama ya wilaya ya Bukombe.

Jaji Mkuu alifafanua kuwa katika wilaya zote Tanzania bara, wilaya zenye majengo ya Mahakama za wilaya ni 37 tu na zilizobaki 102 zinatumia majengo ya kupanga au kwa kuazimwa na Taasisi nyingine za serikali kuu au halmashauri za wilaya.

Alisema moja ya mikakati iliyowekwa na Mahakama ni kuhakikisha kuwa kila eneo jipya la kiutawala linaloanzishwa inajengwa Mahakama kwa kuwa huduma za Mahakama ni muhimu kama ilivyo huduma nyingine.

Awali akitoa Taarifa ya miradi ya ujenzi wa majengo hayo, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania Bwn. Mathias Kabunduguru alisema miradi hiyo mikubwa imetekelezwa na kampuni ya MOLADI TANZANIA LTD, chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU).

 

 

 

 

 

Comments (1)

  • Photo Loading... Obadia kaluta kiiza

    Mhe, Jaji mkuu Nina kushuru na kuku pongeza kwa juhudi zako za kumuunga mkono Ra is wetu mpendwa Jpm mungu awaongezee nguvu na busara .

    03-01-2020

Leave a Comment