Post Details

RAIS AVIAGIZA VYOMBO VYA UTOAJI HAKI KUSHIRIKIANA NA MAHAKAMA

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Chato, Geita

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vyote vya utoaji haki nchini kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili kuhakikisha watanzania wanapata haki kwa wakati.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato alioufanya leo wilayani humo, Rais Magufuli amesema kuchelewa kumalizika kwa mashauri pamoja na mlundikano wa mahabusu magerezani hakusababishwi na Majaji au Mahakimu bali unasababishwa na baadhi ya wadau wa Mahakama wakiwemo Wapelelezi, Waendesha Mashitaka na Mawakili.

“Polisi, wapelelezi, Magereza, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mawakili shirikianeni na Mahakama ili kurahisisha utoaji wa haki”, alisisitiza Rais Magufuli. 

Aidha, Mhe. Rais ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikia ya ujenzi wa majengo ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini. Amesema kujengwa kwa Majengo haya kutasogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi na pia kutasaidia kupunguza idadi ya Mahabusu magerezani kwani huduma zitakuwa zikitolewa kwa wakati.

Amesema licha ya ujenzi wa majengo ya kisasa, Mahakama ni zaidi ya majengo hivyo ameahidi kushughulikia changamoto ya upungufu wa watumishi wa Mahakama. Alisema, Serikali inajitahidi kuongeza idadi ya watumishi wa Mahakama wakiwemo Majaji na Mahakimu. Jumla ya Mahakimu 396 wameajiriwa na kufanya idadi ya Mahakimu kufikia 938 nchi nzima. Kwa upande wa Majaji, alisema jumla ya Majaji 50 wameteuliwa hivi karibuni na kufanya idadi yao kuwa zaidi ya 100.   

Rais Magufuli pia amewata watumishi wa Mahakama nchini kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu na kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuwa wananchi bado wana imani na Mahakama ya Tanzania.   

Awali akimkaribisha Mhe. Rais, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama nchini kufanya kazi kwa bidii na kufuata maadili ili kuleta tija katika kuwahudumia wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki.

Katika kuboresha miundombinu ya Mahakama, Jaji Mkuu alisema hivi sasa Mahakama inaendelea kutekeleza miradi 33 ya ujenzi wa majengo ya Mahakama za wilaya na Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini. Aliongeza kuwa jumla ya majengo ya Mahakama tatu za Hakimu Mkazi yamekamilika katika mikoa ya Geita, Njombe, Simiyu, Manyara na Kibaha. Alisema Mahakama pia imekamilisha ujenzi wa majengo 13 ya Mahakama za Wilaya zikiwemo Chunya, Kasulu, Kondoa, Bagamoyo, Mkuranga, Kigamboni, Ilala, Bariadi, Chato, Longido, Ruangwa, Kilwa na Bukombe.

Jaji Mkuu Mkuu kesho anatarajiwa kuzindua jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita pamoja na jengo la Mahakama ya wilaya ya Bukombe.

 

Comments (0)

Leave a Comment