Post Details

‘MAHAKAMA YA RUFANI KUWA MFANO BORA WA MABADILIKO’

Published By:faustine.kapama

  • Jaji Mkuu ahimiza Watanzania kushiriki sensa

Na Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza viongozi wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kuchukua jitihada mahususi ili kuifanya Mahakama hiyo kuwa ya mfano katika mabadiliko, hususani katika matumizi ya teknolojia kwenye utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 5 Agosti, 2022 alipokuwa akifunga Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani uliofanyika katika Hoteli ya Nashera mjini hapa.

“Msajili na Mtendaji wa Mahakama mnao wajibu wa kugeuza Mahakama ya Rufani kutoka kwenye matumizi makubwa ya karatasi na kuwa Mahakama inayotumia vifaa vya kisasa kusikiliza mashauri yanayowasilishwa katika Mahakama ya Tanzania,” amesema.

Jaji Mkuu aliwakumbusha viongozi hao pamoja na wajumbe wa Mkutano kuwa katika mada yake aliyowasilisha, Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw. Kalege Enock aliwaomba kuwa kama viongozi wanayo nafasi ya kuonyesha mifano kwa wengine na vile vile kuwa sehemu ya kuangalia upya taratibu za kimahakama na kuziweka kwenye mifumo ya kimtandao.

“Lazima mtafute majibu kwa nini usajili wa mashauri umefika asilimia 98 kwa njia ya mtandao, lakini mara baada ya kupokelewa kwa njia hiyo tunarudi tena kwenye makaratasi. Hilo ndiyo suala la ajabu kidogo. Haya ni maeneo ambayo Mahakama ya Rufani tunaweza kuwa mfano kwa mabadiliko,” alisema.

Mhe. Prof. Juma, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo akahoji, “Kwa nini hatuna electronic files (majalada ya kielektroniki), nadhani mada zilizotolewa zinatuhimiza kwamba tuanze kuhama kutoka matumizi ya karatasi twende katika matumizi ya Mahakama mtandao.”

Amesema pia kuwa kama alivyoeleza katika hotuba yake ya ufunguzi, Majaji wa Mahakama ya Rufani ni viongozi ambapo kiongozi mzuri huwa hasubiri kuambiwa, bali anao wajibu wa kuuliza na kufuatilia popote pale penye changamoto ya aina yoyote kwa kuzingatia viongozi wa sasa wa Mahakama wapo wazi na wanapokea changamoto zote na pamoja na ushauri.

“Ni matarajio yangu kwenu pamoja na wajumbe wote wa Mkutano kwamba ninyi kama viongozi hamtasubiri kuambiwa na sekretarieti kuwa wamefanya nini bali ni wajibu wetu pia kufuatilia yote tuliyokubaliana kama yote yanatekelezwa na sisi wenyewe au wengine wanaotakiwa kutekeleza,” alisema.

Amewaomba wajumbe kuwashirikisha watumishi wengine wa Mahakama ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria Mkutano huo ambao umekuwa na manufaa makubwa na kuwasihi wanapokumbana na changamoto ya kiutendaji wajitahidi kuiwasilisha katika mamlaka husika haraka ili ipatiwe ufumbuzi.

Jaji Mkuu alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wajumbe kuhusu zoezi la sensa ambalo litafanyika terehe 23 Agosti, 2022 nchini kote. “Zoezi hili ni muhimu sana kwetu sisi Mahakama kwa sababu mipango yetu mingi ya ujenzi wa miundombinu kupeleka huduma kwa wananchi itategemea matokeo ya hiyo sensa, hivyo tuwahimize watumishi, ndugu zetu na marafiki washiriki hilo zoezi,” amesema.

Kadhalika, Mhe. Prof. Juma alisisitiza kuwa kwa Mahakama zoezi la sensa linawakumbusha umuhimu wa kukusanya takwimu muhimu kama shughuli zao za kila siku ambazo zinatakiwa kuwasaidia kufanya uamuzi wa kisera na ule wa uboreshaji.

Amesema awamu ya pili ya mradi wa Benki ya Dunia imetambua umuhimu wa kukusanya takwimu na inaunga mkono kuanzishwa kwa Kituo cha Matukio cha Mahakama ya Tanzania ambacho kitakuwa kinapokea data na takwimu kuhusu masuala mbalimbali yanayotokea mahakamani.

“Moja ya eneo ambalo mradi wa uboreshaji umeagiza kitengo cha uboreshaji kufanya ni kuwezesha uwepo wa gender justice strategic framework. Kituo hiki ni muhifadhi wa taarifa hizo muhimu ambazo zinatakiwa kutusaidia na wao wamesisitiza kwamba tuanze kukusanya taarifa za haki jinsia,” alisema Jaji Mkuu.

Kwa mujibu wa Mhe. Prof. Juma, Mahakama ya Tanzania inatakiwa kukusanya takwimu kuhusu gender justice (haki jinsia), gender violence (ukatili wa kijinsia) ambapo Andiko linatakiwa kutayarishwa kusaidia ukusanyaji wa takwimu, eneo ambalo mradi wa Benki ya Dunia utapimwa.

Jaji Mkuu amesema kuwa takwimu za haki jinsia kutoka katika mashauri yanayopitia mahakamani, wananchi wanaohudhuria mahakamani na malalamiko yanayopokelewa mahakamani zinatakiwa vile vile kukusanywa kwa kuzingatia haki jinsia.

“Kwa mfano, katika kila Mahakama tuna vituo vya madawati ya jinsia ambavyo vinakusanya taarifa kila siku, lakini hatujui hizo taarifa zinakwenda wapi, zinashughulikiwaje na zinasaidia nini katika kuboresha sera na mambo ya kiutawala ya Mahakama. Kwa hiyo, tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunatumia hizo takwimu kuboresha hali ya haki jinsia,” amesema.

Mkutano huo ambao uliwaleta pamoja Majaji wote wa Mahakama ya Rufani, Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Kevin Mhina, ambaye ndiye alikuwa Katibu, Naibu Wasajili na watumishi wote kutoka katika Mahakama hiyo ulifunguliwa jana tarehe 4 Agosti, 2022 na Jaji Mkuu ambapo wajumbe walipata nafasi ya kupokea taarifa kuhusu hali ya mashauri na utendaji.

Kadhalika wajumbe wa Mkutano huo ambao uliwashirikisha viongozi wengine wa Mahakama kama waalikwa walipitishwa kwenye mada mbalimbali zilizotolewa na wawezeshaji wabobezi, akiwemo Jaji wa Mahakama ya Rufani mstaafu, Mhe. Edward Rutakangwa.

Miongoni mwa viongozi wa Mahakama walioalikwa kwenye Mkutano huo ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.

Comments (0)

Leave a Comment