Post Details

UPOTEVU WA MAJALADA, NYARAKA MAHAKAMANI KUWA HISTORIA

Published By:faustine.kapama

  • Mahakama ya Tanzania haina mpinzani ufuatiliaji hukumu kwenye mtandao

Na Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro

Mahakama ya Tanzania imeanzisha mifumo mbalimbali inayosaidia kurahisisha huduma za utoaji wa haki, ikiwemo ule unaothibiti upotevu wa majalada na nyaraka mahakamani, hatua inayoodoa kabisa malalamiko kutoka kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha TEHAMA cha Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Hali ya Mifumo ya TEHAMA na Matumizi ya TEHAMA kuelekea Mahakama Mtandao katika siku ya pili ya Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani unaofanyika mjini hapa.

Amewaambia wajumbe wa Mkutano huo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwa mfumo mpya wa Mahakama umejengwa kwa kuzingatia viwango vya kiusalama vilivyowekwa kwa mamlaka ya Serikali Mtandao nchini Tanzania na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na miongozo mbalimbali katika ujenzi wa mifumo.

“Mfumo huu utakuwa na uwezo wa kutunza kumbukumbu za namna ambazo watumiaji wake wameingia na kufanya nini. Hivyo taarifa zote zitahifadhiwa zikionyesha kila mtumiaji aliyeingia kwenye mfumo amefanya kitu gani,” amesema.

Akijibu moja ya hoja iliyoibuliwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani waliokuwa wanatoa hoja mbalimbali kwenye Mkutano huo, Bw. Enock alifafanua kuwa watu wote ambao watakuwa wanaingia kwenye mfumo ni wale ambao watakuwa wameruhusiwa kwa mujibu wa nafasi za vyeo vyao ama kazi zao mahakamani.

“Watajaza fomu maalumu ambayo itahifadhiwa kwenye majalada yao, lengo ni kuongeza uwajibikaji ili kila mtumiaji awajibike  namna anavyotumia mfumo kwa ajili ya kuepusha matumizi mabaya ya mtandao na pia upotevu wa nyaraka na mambo mengine yanayofanana na hayo. Kwa hiyo kutakuwepo na uwajibikaji mkubwa sana,” amesema.

Bw. Enock amewaeleza wajumbe wa Mkutano huo kuwa Mahakama ya Tanzania ni kati ya Taasisi chache za umma ambazo zimefungamanisha TEHAMA na shughuli zake za utendaji (business operations).

Mkurugenzi huyo amesema kuwa Mpango Mkakati wa Mahakama wa kwanza (2015/16 - 2019/20 uliweka dira na mikakati inayolenga kuongeza ufanisi kwa kutumia TEHAMA na uliainisha vipaumbele vya TEHAMA; miundombinu ya mawasiliano, kusimika vifaa vya kuendeshea mashauri na kuimarisha masijala

“Mahakama ya Tanzania imekamilisha kufanya mapitio ya mtiririko wa utendaji kazi (business process re-engineering) ya huduma za Mahakama (Court Services) ambapo utendaji kazi uliopo sasa una jumla ya hatua 703 na baada ya zoezi la mapitio zitabaki hatua 320 ambayo ni sawa na asimilia 46 ya ongezeko la ufanisi,” amesema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amewaambia wajumbe wa Mkutano huo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya uboreshaji, mpango mkakati na awamu ya pili ya mradi wa Benki ya Dunia  kuwa Mahakama ya Tanzania haina mpinzani kwenye ufuatiliaji wa hukumu zilizopandishwa kwenye mtandao.

Mhe. Dkt. Rumisha amesema kwa sasa Mahakama ya Tanzania inashindana na nchi ya Marekani ambapo asilimia 85 ya uamuzi unaotolewa na Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu unapandishwa kwenye mtandao, hivyo kuvuka lengo lililopo.

“Asilimia 82.8 ya uamuzi uliopandishwa kwenye mtandao kutoka Tanzania unafuatiliwa ikifuatiwa na Marekani yenye asilimia 2.7 tu. Majirani zetu hawaelewi kabisa tunafanyaje, sio Kenya wala hata Afrika ya Kusini,” amesema.

Mkuu huyo wa Kitengo cha Uboreshaji amebainisha pia kuwa Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani kutokana na kasi ya usikilizaji wa mashauri mbalimbali.

Ametolea mfano muda wa kusikiliza mashauri, kwa mwaka 2015 ilikuwa siku 515, lakini kwa mwaka 2021 umepungua hadi siku 119 tu. Amesema Mahakama inayotembea ndiyo kabisa, imefanya miujiza ambapo mashauri yanamalizika kwa siku 30 tu badala ya siku 120 kwa Mahakama za kawaida.

“Kwa sasa tupo kwenye tarakimu moja tofauti na nchi zingine zinazotuzunguka. Mrundikano ulipungua hadi asilimia 8.4 ilipofika mwaka 2021. Uboreshaji wa data uliwezesha ufuatiliaji bora na afua za kimkakati na tumevuka malengo kwenye mashauri ya kibiashara na trafiki,” amesema.

Mada zingine zilizowasilishwa katika siku hiyo ya pili kabla ya Mwenyekiti kufunga Mkutano huo zilihusu maandalizi ya kustaafu utumishi wa umma, maelezo na ufafanuzi kuhusu kanuni mpya za ukokotozi wa pensheni kwa watumishi wanaostaafu na dondoo za afya na ugonjwa wa UVIKO-19.

Comments (0)

Leave a Comment