Post Details

KASI USIKILIZAJI MASHAURI MAHAKAMA YA RUFANI HATARI

Published By:faustine.kapama

  • Mahakama haishikiki uboreshaji miundombinu

Na Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro

Kasi ya kumalizika kwa mashauri (clearance rate) katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania imepanda kutoka asilimia 73 kwa Disemba 2021 mpaka kufikia asilimia 92.9 mpaka Juni 2022.

Hayo yamebainishwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mashauri katika Mahakama hiyo kwenye Mkutano wa Nusu Mwaka ambao umefunguliwa leo tarehe  Agosti, 2022 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

“Kiwango cha kumaliza mashauri kwa kipindi cha mwezi Januari-Juni 2022 kilikuwa ni asilimia 92.9. Hivyo Mahakama ya Rufani kwa kipindi cha Januari-Juni 2022 ilikuwa na uwezo wa kumaliza asilimia 92.9 ya mashauri yanayosajiliwa. Iwapo kama katika kipindi hicho uamuzi wote ungetolewa kiwango cha kumaliza mashauri kingekuwa asilimai 97. Katika kipindi cha mwaka jana  ilipofika Disemba 2021 kiwango cha kumaliza mashauri ilikuwa ni asilimia 73. Hivyo kasi ya kumaliza mashauri imepanda kwa asilimia 19.9,” amesema.

Mhe. Mhina ameueleza Mkutano huo unaofanyika katika Hoteli ya Nashera mjini hapa kuwa Mahakama ya Rufani ilianza mwaka mpya wa 2022 ikiwa na jumla ya mashauri 5,054 ambayo yalibaki mwaka 2021. Amesema kuwa Januari - Juni 2022, Mahakama hiyo ilisajili jumla ya mashauri 908 na kati ya hayo 237 ni yenye asili ya jinai na 671 yenye asili ya madai.

Kwa mujibu wa Mhe. Mhina, ambaye ni Katibu wa Mkutano huo, mashauri yaliyosikilizwa yalikuwa 881 yanayojumuisha 313 ambayo ni ya jinai na mengine 568 ya madai. “Kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka uliopita (Janauri-Juni 2021) jumla ya mashauri 734 yalisikilizwa hivyo kuna ongezeko la mashauri 147 yaliyosikilizwa,” amesema.

Akizungumzia hali ya utoaji haki katika Mahakama hiyo ya juu hapa nchini, Mhe. Mhina amebainisha kuwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022 kwa mujibu wa kalenda ya Mahakama ya Rufani, Mahakama ilipanga kufanya vikao 16 katika kanda 12 ambazo ni Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza, Iringa, Tabora, Mtwara, Dodoma, Tanga, Musoma, Kigoma na Zanzibar.

“Vikao vyote vilifanyika kwa asilimia 100 kama vilivyokuwa vimepangwa. Katika kipindi husika Mahakama ya Rufani ilikuwa na majopo saba (7). Majopo hayo yaliketi mara 28 katika vikao 16 vilivyokuwa vimepangawa. Majaji  wa Rufani 24 akiwemo na Jaji Mkuu walishiriki vikao hivyo. Jumla ya mashauri yaliyopangwa yalikuwa 1,003, yaliyosikilizwa yalikuwa 881 na yaliyoahirishwa ni 122,” amesema.

Amezitaja baadhi ya sababu zilizopelekea kuahirisha kwa mashauri hayo kama Mawakili au warufani kuomba kuwasilisha nyaraka za ziada au nyongeza (supplementary record(s), hati za kuchelewa au kufungua rufaa au maombi nje ya muda (certificate of delay) kutokuwa sahihi, kutofika mahakamani kwa warufani kutokana na sababu mbalimbali au kutopatikana, kufariki kwa warufani  na kuahirisha ili kupisha msimamizi au wasimamizi wa mirathi wateuliwe na kuunganishwa kwenye rufaa.

Msajili huyo ametaja mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika kipindi husika ikiwemo kuendelea kupungua kwa mashauri ya mlundikano kutoka mashauri 707 (14%) Disemba 2021 mpaka mashauri 611 (11%) Juni 2022 na kuongezeka kwa kiwango au kasi ya kumalizika kwa mashauri (clearance rate) kutoka asilimia 73 Disemba 2021 mpaka kufikia asilimia 92.9 mpaka Juni 2022.

Amesema pia kuwa kumekuwepo na hali ya kupungua kwa mzigo wa mashauri kwa jopo (workload) kutoka mashauri 917 kwa jopo Disemba 2021 mpaka kufikia mashauri 859, kufanya vikao vyote kwa asilimia 100 kama ilivyopangwa katika kalenda ya Mahakama ya Rufani na kuendelea kupungua kwa mashauri yanayo ahirishwa kutoka mashauri 150 kwa kipindi cha Jan-Juni 2021 mpaka kufikia mashauri 122 kwa kipindi cha Jan-Juni 2022.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Steven Magoha aliwasilisha taarifa ya utendaji ya Mahakama ya Rufani kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Solanus Nyimbi ambayo imesheheni mambo mengi, ikiwemo jitihada zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania kuboresha na kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi.

Bw. Magoha ameuambia Mkutano huo kuwa Mahakama ya Tanzania imeendelea na utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26) wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Mahakama, ambapo katika mwaka 2021/2022 jumla ya miradi 60 ilitekelezwa katika ngazi mbalimbali.

“Miradi ya Ujenzi iliyokamilika ni pamoja na Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (6) katika Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Morogoro, Mwanza na Dodoma, ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi tatu (3) za Njombe, Katavi, Lindi, ujenzi wa Mahakama za Wilaya sita (6) za Bahi, Chemba, Rungwe, Makete, Wanging’ombe na Bunda na ujenzi wa Jengo la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto,” amesema.

Ametaja miradi mingine kama ujenzi wa Mahakama za Mwanzo sita(6) za Matiri-Mbinga, Hydom-Mbulu, Ngerengere-Morogoro, Mtae-Lushoto, Kibaigwa-Kongwa na Lugarawa-Ludewa, ujenzi wa nyumba mbili (2) za Mahakimu Loliondo-Arusha na ujenzi wa Jengo la kuhifadhi Kumbukumbu-Tanga.

Bw. Magoha ametaja miradi inayoendelea kwa sasa kuwa ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Songwe na Mahakama za Wilaya nane (8) za Nanyumbu, Namtumbo, Same, Tandahimba, Kilindi, Sikonge, Mwanga na Ngara na ujenzi wa Mahakama za Mwanzo sita (6) za Chanika (Ilala), Kabanga (Ngara), Kimbe (Kilindi), Nyakibimbili (Bukoba), Mlimba na Mang’ula (Morogoro).

Amesema pia kuwa kuna ukarabati wa Jengo la Mahakama Kuu Tabora na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, ujenzi wa Mahakama za Wilaya 18 katika Wilaya za Kakonko, Buhingwe na Uvinza (Kigoma), Butiama na Rorya (Mara), Itilima na Busega (Simiyu), Songwe (Songwe), Mbogwe na Nyang’wale (Geita), Kyerwa na Misenyi (Kagera), Gairo, Mvomero na Kilombero (Morogoro), Mkinga (Tanga), Tanganyika (Katavi) na Kaliua (Tabora) na Ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama na Nyumba za Majaji Dodoma.

Comments (0)

Leave a Comment