Post Details

RAIS AWATAKA MAJAJI KUTOA HUKUMU KWA HAKI NA KWA WAKATI

Published By:Mary C. Gwera

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Majaji aliowateua na kuwaapisha leo kufanya kazi kwa haki na kutoa hukumu kwa wakati.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Viongozi wengine aliowateua, leo Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amewapongeza Majaji hao na kuwataka kutekeleza wajibu wao ili  wananchi wapate haki kwa wakati.

“Haki hutolewa na Mungu lakini ninyi mmepewa mamlaka makubwa hapa duniani ya kuhukumu hivyo katoeni hukumu kwa haki na msicheleweshe haki”, alisema Mhe. Rais.

Aidha Mhe.Magufuli amewataka Majaji wapya kutimiza wajibu wao kwa haki na kuwatumikia watanzania hasa wale wanyonge ambao haki zao zinapotea.

Akimzungumzia aliyekuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati, Mhe. Rais alimpongeza kwa kazi nzuri aliyofanya akiwa Mahakama ya Tanzania na kumtaka akasaidie kuusimamia mkoa wa Njombe wenye fursa nyingi ili mkoa huo usonge mbele. 

Awali akizungumza, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alimshukuru Mhe. Rais kwa kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania hatua itakayosaidia mashauri kumalizika kwa wakati.

Alisema hivi sasa idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania imefikia 78 kutoka Majaji 66 waliokuwepo kabla ya uteuzi wa jana. Alisema Majaji wawili wanatarajia kustaafu mwishoni mwa mwaka huu na idadi yao itabaki kuwa ni Majaji 76 ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

Alisema kulingana na idadi hiyo ya Majaji, kila Jaji hivi sasa ana mzigo wa kusikiliza mashauri zaidi ya 500 wakati uwezo wa Jaji mmoja ni kusikiliza mashauri 220 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Aliwataka Majaji walioapishwa leo kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria kwa kuwa Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu wa kujisimamia  katika kazi ambapo kila Jaji anatakiwa kusikiliza na kumaliza mashauri 220 kwa mwaka, kutoa nakala za hukumu ndani ya siku 21 tangu kumalizika kwa shauri na kutoa mwenendo wa shauri ndani ya siku 30.

“Mnaanza kazi kwa kuaminiwa, Mhe. Rais amewaamini na mmeibeba imani, hivyo iendelezeni imani hiyo kwani ikipungua tutatumia sheria”, alisisitiza Jaji Mkuu.

Akimzungumzia aliyekuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Jaji Mkuu alimpongeza kwa kazi nzuri aliyofanya ndani ya Mahakama na kumtaka kwenda kuendeleza kazi hiyo nzuri pia katika mkoa wa Njombe.

Jana Rais Magufuli alifanya uteuzi wa Majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na viongozi wengine wakiwemo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),   Katibu Tawala Mkoa wa Njombe (RAS), Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Kamishna wa kazi, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Makamu wake pamoja na Makamishna wa Tume hiyo.

Comments (0)

Leave a Comment