Post Details

JAJI MKUU: MSIKUBALI KUINGILIWA KATIKA MAMLAKA ZENU

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaasa Mahakimu Wakazi wapya kutokubali maelekezo ya aina yoyote kutoka nje ya Mamlaka zao kuhusiana na mashauri yaliyopo mbele yao.

Akizungumza na Mahakimu Wakazi wapya 23 mara baada ya kuwaapisha rasmi, mapema Novemba 01, 2019 katika Ukumbi wa Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa Mahakimu hao wana mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri bila kuingiliwa na yeyote.

“Jaji au Hakimu lazima awe ni mtu wa kuheshimu mamlaka nyingine, vivyo hivyo msikubali maelekezo ya aina yoyote kutoka nje ya Mahakama ama iwe Jaji au mtu mwingine kuhusiana na kesi/mashauri yaliyopo mbele yenu,” alieleza Mhe. Jaji Prof. Juma.

Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka Mahakimu hao kutekeleza majukumu yao bila upendeleo kwa kuwa ni jambo linalosababisha matabaka baina ya watu/wananchi.

“Upendeleo ni jambo la hatari sana, muwe wawazi, muwe wasikilizaji makini, lazima muwasaidie wananchi ambao wengi hawajui sheria kwa kuwaelimisha,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.

Hali kadhalika, Mhe. Jaji Mkuu aliwapa angalizo Mahakimu hao juu ya uandishi wa hukumu sahihi kwa kutumia lugha inayoeleweka ili wananchi/wateja waweze kuelewa kwa urahisi.

Masuala mengine aliyowaeleza Mahakimu hao ni pamoja na kufanya tafiti, matumizi ya TEHAMA na kuishi viapo vyao wanapotekeleza majukumu yao.

Jumla ya Mahakimu Wakazi wapya 23 wameapishwa na wamepangiwa kufanya kazi katika Mahakama za Mwanzo katika mikoa mbalimbali nchini.

Comments (0)

Leave a Comment