Post Details

JAJI MFAWIDHI MAHAKAMA KUU DIVISHENI BIASHARA AHIMIZA MATUMIZI YA TEHAMA

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe.Patricia Fikirini amewataka Majaji, Naibu Wasajili, Wasaidizi wa Kisheria wa Majaji na watumishi wengine wa Mahakama hiyo kuwa mstari wa mbele katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha uendeshaji wa mashauri yanayohusu masuala ya kibiashara.

Hayo yalisemwa na Jaji Fikirini  Oktoba 30, mwaka huu  wakati akifungua mafunzo elekezi ya siku mbili (2) kwa Majaji  na Naibu Wasajili wa Mahakama hiyo, yanayoendelea  katika ukumbi wa Kituo cha Mafunzo na Habari, kilichopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

“Tunatakiwa tubadilike kwa haraka ili tuendane na mabadiliko ya mazingira ya kibiashara yanayotokea ndani na nje ya nchi. Pia ujio wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, inaweza kujumishwa kwamba usimamizi na usikilizaji wa mashauri umekuwa rahisi. Hivyo ili kuweza kufanya mabadiliko haya yatokee, tunatakiwa tubadili mitazamo,” alisema Jaji Fikirini.

Jaji Fikirini aliongeza kwamba mafunzo hayo, yanasaidia kubadilisha uzoefu wa kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo katika uendeshaji wa mashauri mbalimbali na vipingamizi, ikiwemo kuweza kuzipatia ufumbuzi, ikiwa ni hatua ya kuweza kuweka mazingira ya biashara na uwekezaji kuwa rafiki nchini.

Aliongeza kuwa wao ndio wanawajibu mkubwa wa kutekeleza majukumu ya Mahakama hiyo, hivyo uelewa na utumiaji sahihi wa taratibu na kanuni ambazo ni maalum kwa Mahakama ya Biashara ni muhimu.

Katika mafunzo hayo, mada zilizotolewa leo ni uanzishaji wa Mahakama ya Biashara na umuhimu wake, ambayo ilitolewa na Jaji Mstaafu, Mhe. Prof. John Ruhangisa, Usimamizi wa Mahakama hiyo, mwezeshaji alikuwa ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mtwara, Mhe. Angelo Rumisha na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA), iliyotolewa na  Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock.

Comments (0)

Leave a Comment