Post Details

MATUMIZI YA TEHAMA KURAHISISHA UFANYAJI TAFITI

Published By:Mary C. Gwera

Imeelezwa kuwa usambazaji wa taarifa za Kimahakama kwa wakati kwa Kutumia Tovuti, Maktaba Mtandao ‘e-library’ pamoja na Tanzlii itawarahisishia wadau wa ndani na nje ya Mahakama kufanya tafiti kwa urahisi.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mhadhiri kutoka katika taasisi ya sheria Africa (AFRICANLII), Bi. Mariya Bright wakati akitoa mafunzo ya taarifa za kisheria na maamuzi kwa kutumia teknolojia katika mifumo ya Mahakama yanayofanyika nchini South Afrika katika Mji wa Cape Town.

“Mafunzo haya yatasaidia sana kuwapa maarifa washiriki katika kufanya tafiti za kisheria, kujua kama tovuti zinazotoa taarifa za kisheria zinakidhi haja ya wadau ama nini kifanyike ili kufanya mifumo ya Kimahakama kutoa taarifa muhimu kwa wadau wote wa sheria  na kwa wakati,” alieleza Bi. Bright.

Mbali na kuelezea umuhimu wa mafunzo hayo, Mhadhiri huyo pia alitoa mafunzo ya jinsi ya kutumia Kitambaza (scan) maalum kiitwacho seuz ambacho kina uwezo wa kutambaza (scan) vitabu vizuri na kusaidia pia kurefusha uhai wa kitabu kikiwapo katika nakala laini kuliko kikiwa katika nakala ngumu.

Mafunzo hayo yanayoendelea katika ukumbi wa Mikutano katika Chuo Kikuu cha Cape Town kilichopo nchini Afrika Kusini yataleta tija katika Mahakama ya Tanzania hasa katika maboresho ya huduma ya utoaji haki yanayoendelea kufanyika.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) yaliyoanza Oktoba 28, 2019 hadi Novemba 01, mwaka huu yameshirikisha nchi kumi (17) za Afrika zilizopo katika mfumo wa (LII-Legal Information Institutes) ikiwemo Tanzania ambayo imewakilishwa na Watumishi kutoka Mahakama akiwemo Mhe. Kifungu Mrisho ambaye ni Hakimu Mkazi na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maktaba ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Israel Kamendu, Afisa Tehama na Bw. Salum Tawani, Afisa Maktaba.

Comments (0)

Leave a Comment