Post Details

MALALAMIKO YANAYOTOKEA KWENYE MABARAZA YA ARDHI YANAICHAFUA MAHAKAMA: JAJI KIONGOZI

Published By:LYDIA CHURI

Na Faustine Kapama– Mahakama,         Songea

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amezishauri mamlaka zinazosimamia uendeshaji wa Mabaraza ya Ardhi kutoa uwezeshaji wa kutosha ili yaweze kutimiza majukumu yake kikamilifu kwani malalamiko yanayokuja mahakamani kutokea kwenye taasisi hizo yanaichafua Mahakama ya Tanzania.

Mhe. Siyani ameyasema hayo katika siku ya mwisho ya ziara ya Tume ya Utumishi wa Mahakama chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambayo leo tarehe 23 Juni 2022 imetembelea Mkoa wa Ruvuma kuzungumza na watumishi, wadau mbalimbali wa Mahakama na Wenyeviti wa Kamati za Maadili kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya.

“Wizara na Mamlaka zinazaosimamia Mabaraza hayo zinatakiwa kuyawezesha kufanya kazi kwa kuongeza utendaji, kuwapa vitendea kazi na kusimamia nidhamu na uadilifu. Yapo maeneo tumepita katika ziara hii, yupo Mwenyekiti mmoja anahudumia Mkoa mzima. Kwa hiyo malalamiko yatakuja tu na malalamiko dhidi ya Mabaraza ni malalamiko ya Mahakama,”amesema.

Akieleza matarajio ya Mahakama kwa wadau mbalimbali katika myororo wa utoaji haki nchini, Mhe. Siyani amesema kuwa Mabaraza ya Ardhi yamekuwa ni sehemu ya malalamiko yanayopokelewa dhidi ya Mahakama na kwamba wananchi hawajui tofauti kati ya Baraza la Ardhi na Mahakama.

“Kwa hiyo, asipotendewa haki analalamika dhidi ya Mahakama na msingi wa malalamiko hayo ni lile takwa la kikatiba kwamba Mahakama ndiyo iliyopewa kauli ya mwisho ya kutoa haki. Kwa hiyo, akiona katendewa ndivyo sivyo anajua Mahakama ndiyo ambayo haijamtendea haki,” amesema.

Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi, kwa sasa Mahakama haiwezi kuwa mbali na malalamiko hayo na kama Mabaraza ya Ardhi hayataimarishwa na utendaji wake kupimwa hali hiyo itaendelea.

Akaeleza matarajio ya Mahakama kwa mdau huyo kuwa Mabaraza hayo hayatakwamisha kasi ya usikilizaji wa rufaa na mapitio ya mashauri ya migogoro ya ardhi kwa kuhakikisha kumbukumbu au majalada ya mashauri hayo yanawasilishwa haraka iwezekanavyo katika Mahakama Kuu yanapoitishwa.

Kwa upande wa wananchi, Mhe. Siyani amebainisha kuwa Mahakama inatarajia kwa mdau huyo ambaye pia ni muhimu kushiriki uboreshaji unaoendelea kwa kuacha kushawishi rushwa kwa watumishi wa Mahakama na hata wao wakiombwa kukataa kutoa rushwa na badala yake watoe taarifa za kweli kwenye mamlaka husika kuhusu vitendo hivyo vya ukosefu wa maadili.

Amewaomba wananchi kuondokana na hisia za rushwa hata kama hawajaombwa na hata kama mazingira kuwa yameboreshwa na hakuna rushwa, lakini bado baadhi yao wanafikiri hawawezi kupata huduma mahakamani bila kutoa rushwa.

“Kazi kubwa imeshafanyika sasa hivi na niwaombe wananchi na wadau wote kuanza kuondokana na dhana kwamba huwezi kupata haki mahakamani mpaka utoe rushwa, tumehama huko, hatuko tena. Tunataka kuwa na taasisi ambayo hainyoshewi vidole. Hatutaki kuwa miongoni mwa taasisi ambazo zinahusishwa na ukosefu wa maadili,” alisema.

Jaji Kiongozi aliwageukia Mawakili wa Kujitegemea kwa kuwataka kuacha kutumia mbinu za kiufundi kama mapingamizi ya awali wakati wa kusikiliza mashauri katika Mahakama za Mwanzo, hatua ambayo itasababisha ucheleweshaji, hivyo kuwanyima wananchi kupata haki zao kwa wakati.

Amebainisha kuwa kufuatia marekebisho ya sheria, sasa hivi Mawakili wanaruhusiwa kutoa huduma kwenye Mahakama za Mwanzo hapa nchini, lakini changamoto ambayo imejitokeza ni kuona wanakwenda katika Mahakama hizo katika mwendo ule ule walionao kwenye Mahakama zingine walizokuwa wanahudumu kuanzia Mahakama za Wilaya mpaka Mahakama Kuu.

“Matokeo yake ni kwamba mbinu za kiufundi zinatumika sana katika Mahakama za Mwanzo. Hizi Mahakama kama mlivyomsikia Jaji Mkuu zinapokea zaidi ya asilimia 70 ya mashauri yote katika nchi yetu. Msingi mkubwa katika Mahakama hizi ni mapatano katika kufikia haki. Ni matarajio ya Mahakama kuwa uwepo wa Mawakili usiondoe dhana hiyo ya kupatana kwa kutumia zaidi mbinu za kiufundi,” amesema.

Amesema kuwa Mahakimu wanatarajiwa kuonyesha weledi wao na kutumia misingi ya kupatana na maridhiano baina ya wadaawa, hivyo ni matarajio ya Mahakama kuwa uwepo wa Mawakili  kwenye Mahakama hizo hautaathiri kasi ya usikilizaji wa mashauri.

Kadhalika Jaji Kiongozi amesema Mawakili wanatarajiwa kuwa chachu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo Mwenyekiti wa Tume amekuwa akiwapokea Mawakili mara mbili kila mwaka, lakini bado hawajaonyesha mwamko wa moja kwa moja kupokea hizo kauli za matumizi ya teknilojia.

“Hivyo nitoe wito kwa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kushiriki moja kwa moja katika jitihada za Mahakama kuelekea matumizi kamili ya teknolojia katika usikilizaji wa  mashauri. TLS iwajengee uwezo wanachama wake kutumia njia hii na sisi tupo tayari kushirikiana nao kuhakikisha kwamba Mawakili wanakuwa chachu ya uboreshaji katika Mahakama ya Tanzania,” amesema.

Comments (0)

Leave a Comment