Post Details

WATUMISHI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA BIDII

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama wakiwemo Mahakimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii wakati Serikali ikiendelea kushughulikia maslahi yao pamoja na ya watumishi wengine wa Umma.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama jana mkoani Lindi, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alisema maslahi ya Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa Mahakama hayana budi kufanyiwa uboreshaji kutokana na majukumu mazito waliyonayo ambayo hayaendani na kiwango cha mishahara wanachopata.

Akisisitiza suala la nyongeza ya mishahara kwa Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa Mahakama, Jaji Mkuu akitolea mfano wa Tume ya Jaji Warioba ya rushwa, alisema Tume hiyo katika ripoti yake ya mwaka 1996 kwenye moja ya mapendekezo yake iligusia suala la maslahi madogo kwa Mahakimu.

Kuhusu suala la maadili kwa Mahakimu, Mwenyekiti huyo wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alitoa rai kwa wenyeviti wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya mkoa na wilaya kusimamia maadili ya Mahakimu na kuwaelimisha wananchi kuhusu uwepo wa Kamati hizo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bibi Zainabu Talack ameiomba Mahakama ya Tanzania kuongeza idadi ya Mahakimu katika mkoa huo kwa kuwa waliopo hivi sasa hawatoshi hali inayosababisha Hakimu moja kuhudumia Mahakama zaidi ya moja.

Kuhusu maslahi ya watumishi wa Mahakama wakiwemo Mahakimu, Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa Mahakama haina budi kuwawezesha watumishi hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.

Aliwataka Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa Umma kutumia fursa zilizopo mkoani humo kujipatia kipato cha ziada baada ya saa za kazi.

“Mahakimu wajishughulishe na shughuli za uzalishaji ili wawe na ustawi mzuri utakaowawezesha kufanya kazi zao vizuri”, alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Tume ya utumishi wa Mahakama inaendelea na ziara yake yenye lengo la kujitangaza na kuimarisha Kamati za maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya mkoa na wilaya katika mikoa ya Lindi na Ruvuma.

Comments (0)

Leave a Comment