Post Details

JAJI MKUU: KEMEENI MAAHIRISHO YA KESI BILA SABABU ZA MSINGI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Naibu Wasajili na Mahakimu kutoruhusu maahirisho ya mashauri ya mara kwa mara bila ya sababu za msingi.

Akizungumza na Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya mara baada ya kuwaapisha Naibu Wasajili na kuwakabidhi nyenzo za kazi Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya mapema Oktoba 25, 2019 katika Ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu-Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa wana nguvu/mamlaka ya kuhakikisha kuwa mashauri yanakwisha kwa muda unaotakiwa.

“Nyie mna mamlaka ya kuwadhibiti Wapelelezi, Waendesha mashtaka kuhakikisha wanaharakisha kufanya upelelezi na kufuata sheria na taratibu zilizopo,” alisisitiza Mhe. Jaji Prof. Juma.

Aidha; Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka Maafisa hao wa Mahakama kuhakikisha suala la upelelezi unaofanywa na Polisi linafanyika kwa kutumia ‘video’ kama sheria inavyotaka.

Hali kadhalika, Mhe. Jaji Mkuu amewataka pia Maafisa hao kutumia sheria ya Makubaliano katika kesi za jinai ‘Plea-bargain’ ili kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani.

“Sheria hii ya makubaliano katika kesi za jinai kati ya upande wa mashtaka na mshtakiwa inatumika pia nchini Marekani na imeleta mafanikio katika kupunguza msongamano, hivyo sheria hii isiishie kutumika makao makuu pekee bali itumike katika Mahakama zote nchini,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Mkuu aliwataka Maafisa hao kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi na taratibu za Kimahakama na Taifa kwa kuwa Taasisi imewaamini.

“Ninyi ni viongozi na mtambue kwamba ni injini ya Mahakama kwa aina ya kazi mnazofanya, ni muhimu kufanya kazi kwa kufuata kanuni za Maafisa Mahakama na vilevile ni wajibu wenu kuwaelimisha watumishi mnaowaongoza kujua maadili ya utumishi,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Katika hafla hiyo, Mhe. Jaji Mkuu amewakabidhi nyenzo za kazi jumla ya Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya 10 naye Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewaapisha jumla ya Naibu Wasajili wapya 10 ambao wote wameteuliwa kwa lengo la kuongeza nguvu kazi ya utoaji haki nchini.

Comments (0)

Leave a Comment