Post Details

WADAU-MAHAKAMA YA KAZI WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUONDOA MLUNDIKANO WA MASHAURI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Wajumbe wa Kamati ya utatu ya Mahakama ya Kazi (Tripatite Users Committee) kushirikiana kwa pamoja katika kushughulikia mashauri ya migogoro ya kazi.

Akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Mhe. Jaji Kiongozi katika ufunguzi rasmi wa Kikao cha Kamati ya Utatu kilichofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu-Dar es Salaam, mapema Oktoba 11, 2019, Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Benhajj Masoud alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa mzigo bado ni mkubwa na inahitaji mchango wa wadau wote katika kuyashughulikia mashauri hayo.

“Kwa mwaka 2017, idadi ya mashauri ya kazi yaliyofunguliwa ni 3414, yaliyosikilizwa ni 3135 na yaliyobaki ni 3664, kwa mwaka 2018 idadi ya mashauri yaliyofunguliwa yalikuwa 1944, yaliyosikilizwa ni 2012 na yaliyobaki ni 2256 na kwa mwaka huu 2019 (Januari hadi Agosti) jumla ya mashauri 1889 yamefunguliwa, yaliyosikilizwa ni 1549 na yaliyobaki ni 2549,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.

Hata hivyo; katika hotuba yake, Mhe. Jaji Kiongozi alisema kuwa Mahakama inaendelea na mikakati mbalimbali ya kutatua mlundikano wa mashauri mojawapo ikiwa ni Mhe Jaji Mkuu wa Tanzania kupitia Tangazo lake la Aprili 30, 2018 (Labour Division Judges and Deputy Registrars Designation Notice).

“Kupitia tangazo hili, Mhe. Jaji Mkuu aligatua mamlaka ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa Waheshimiwa Majaji na Naibu Wasajili wote kwenye Kanda zote kasoro Kanda ya Dar es Salaam, kusikiliza mashauri ya kazi,” alifafanua Mhe. Jaji Kiongozi.

Hata hivyo, Mhe. Mgeni rasmi aliwashukuru Wadau kwa mchango mkubwa wanaoendelea kuipatia Mahakama ya Tanzania hususani Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi na kuwataka kupitia kikao hicho kuja na mikakati zaidi itakayotatua changamoto mbalimbali kuhusiana na mashauri hayo.

Aidha; Mhe. Jaji Kiongozi aliwakumbusha Wajumbe hao kuwa jukumu lao kwa mujibu wa Sheria ni kuweka mikakati itakayowezesha kusukuma mbele mashauri.

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi,Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa alisema Serikali inatambua majukumu mazito na mchango mkubwa wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na Wadau wote wa sheria katika utatuzi wa migogoro ya kikazi.

“Serikali inatambua pia kuwa majukumu yenu yana uhusiano wa moja kwa moja na ndoto ya Serikali ya awamu ya tano kuelekea uchumi wa Viwanda kwani wateja wenu yaani wafanyakazi na waajiri ndio wazalishaji wakuu wanaochangia ukuaji wa uchumi,” alieleza Mhe. Ikupa.

Mhe. Waziri huyo pia ameipongeza Mahakama kwa kujipima kupitia wadau wake, kujitathmini namna jamii inavyoitazama na kupendekeza kufanyika kwa mafunzo kuhusu Sheria za kazi kwa Wahe. Majaji na Mahakimu.

Kikao hicho cha siku moja (1) kimeshirikisha Wajumbe wa Kamati ya Utatu kutoka Serikalini, Chama cha Waajiri na Shirikisho la vyama vya wafanyakazi pamoja na wadau wengine wa Mahakama hiyo wakiwemo baadhi ya Majaji Wafawidhi kutoka Kanda mbalimbali, Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu divisheni ya Kazi, Wanasheria na wengineo.

Lengo ni kutathmini kwa pamoja juu ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo pamoja na kuwekeana mikakati mingineyo itakayowezesha kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika kazi ya uondoshaji wa mashauri ya migogoro ya kazi.

Comments (0)

Leave a Comment