Post Details

MAHAKAMA HAITARUDI NYUMA KATIKA MATUMIZI YA TEHAMA

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama, Serengeti

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema Mahakama ya Tanzania haitarudi nyuma katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) hivyo amewataka watumishi wa Mahakama kujifunza ili waweze kutoa huduma bora na kwa wakati.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Serengeti akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Mara, Jaji Kiongozi amesema hivi sasa Mahakama iko kwenye matumizi ya Tehama katika kurahisisha upatikanaji wa Haki na kutoa huduma bora na za haraka kwa wananchi.

Amesema Mahakama inayo mifumo mbalimbali inayorahisisha upatikanaji wa haki na baadhi ya mifumo hiyo ni ule wa kusikiliza mashauri kwa njia ya video (Video Conferencing), mfumo wa kuwatambua Mawakili (TAMS- Tanzania Advocates Management System), na mfumo wa kusajili mashauri (JSDS ll (Judicial Statistics Dashboard System).

Jaji Kiongozi amewataka watumishi wa Mahakama kuwa wepesi katika kujifunza mifumo ya Mahakama na pia kuhakikisha wanapata taarifa mbalimbali za shughuli za Mahakama kupitia mifumo mingine ya Mahakama ikiwemo Tovuti, Blog, Twitter na Facebook.  

“Mahakama haitarudi nyuma kwenye suala la matumizi ya Tehama hivyo muwe wepesi kujifunza na kuliona ni jambo la kawaida kabisa”, alisema Mhe. Dkt. Feleshi.

Awali akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Serengeti Bwn. Nurdin Babu alipomtembelea ofisini kwake, Jaji Kiongozi alisema Mahakama inaendelea  kuboresha huduma zake na jitihada zinafanyika kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa haki kwa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Alisema kupitia Mpango wa ujenzi wa majengo yake unaendelea maeneo mbalimbali nchini, Mahakama pia inao mpango wa kujenga jengo la Mahakama ya wilaya ya Serengeti kama ilivyo kwa wilaya nyingine nchini.

Aidha, Jaji Kiongozi ameliomba jeshi la Polisi kumaliza upelelezi kwenye kesi mbalimbali mapema kwa kuwa kesi nyingi zinazochelewa kumalizika mahakamani ni zile ambazo upelelezi wake huchelewa kukamilika pamoja na zile zinazosubiri kibali cha Mwendesha Mashtaka na ambazo zinasubiri mashahidi.

Akizungumzia kesi zinazohusu mimba za utotoni, Jaji Kiongozi ameshauri matumizi ya kipimo cha DNA ili kesi hizo zisichukue muda mrefu kumalizika na  kuahidi Mahakama kutoa uzito unaostahili katika kesi hizo.

Naye Mkuu wa wilaya ya Serengeti Bwn. Nurdin Babu alisema katika wilaya yake, Serikali inapata ushirikiano mkubwa kutoka Mahakama ya Tanzania na kuiomba Mahakama kuendeleza ushirikiano huo ili wananchi waweze kupata huduma bora.

Alisema ofisi yake inaishukuru Mahakama kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Robonda ambalo awali lilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi na baadaye Mahakama ilikamilisha jengo hilo ambalo hivi sasa linatumika.

Alisema wilaya ya Serengeti inakabiliwa na changamoto ya kuwa na kesi nyingi na hasa zinazohusu nyara za Serikali pamoja na mimba za utotoni kwa watoto wa kike wanaosoma shule za msingi pamoja na sekondari wilayani humo. Alisema kati ya mwezi Januari na Septemba 2019 jumla ya wasichana 13 wenye umri wa chini ya miaka 18 walipata mimba wakiwa mashuleni.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya alielezea changamoto ya gereza la wilaya ya Serengeti ambapo alisema ni dogo ukilinganisha na idadi ya mahabusu waliopo. Gereza hilo lina uwezo wa kuhifadhi mahabusi 216 lakini hivi sasa kuna mahabusu 416 ambao wengi wanatokana na kesi zinazohusu nyara za serikali.

Jaji Kiongozi anaendelea na ziara ya kikazi katika wilaya ya Tarime na baadaye Musoma ambapo atakagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama.

Comments (0)

Leave a Comment