Post Details

‘RC’ KIGOMA AIPONGEZA MAHAKAMA KWA KUSOGEZA HUDUMA YA MAHAKAMA KUU

Published By:Mary C. Gwera

Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kigoma ikiongozwa na  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga imetembelea Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na Nyumba za Makazi za Majaji na kupongeza upatikanaji wa huduma ya Mahakama Kuu katika mkoa huo.

Ugeni huo ulitembelea miradi hiyo ya ujenzi mapema  Oktoba 08, 2019 na ulipokelewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta.

Katika ziara hiyo, Brigedia Jenerali Mstaafu Maganga amepongeza jitihada za Mahakama ya Tanzania katika kusogeza huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwani awali  walikuwa wakisafiri umbali wa takribani  kilomita 858(kwenda na kurudi) kufuata huduma za Mahakama Kuu Mkoani Tabora.

Pia amepongeza utendaji kazi  wa Mkandarasi wa  ‘Masasi Construction Co Ltd’ anayejenga jengo la Mahakama Kuu pamoja na nyumba za Makazi za Majaji.

“Wajumbe wenzangu tuone uwezekano wa kuwatumia wakandarasi hawa katika miradi ya ujenzi kutokana na kazi waliyoifanya katika jengo hili,” alisema Mkuu wa Mkoa

Ziara hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mpango ulioandaliwa na Uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma kuhakikisha wadau wa Mahakama Mkoa wa Kigoma wanapata fursa ya kutembelea jengo hilo jipya na kujionea miundo mbinu iliyopo ikiwa ni pamoja na kupata elimu.

Baadhi ya wadau wakiwemo wajumbe wa Haki Jinai Mkoa, wajumbe wa vituo vya msaada wa kisheria( paralegal) Mkoa wa Kigoma, watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma, wazabuni mbalimbali waliweza kutembelea jengo hilo ambalo linatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Comments (0)

Leave a Comment