Post Details

MAHAKAMA KUPUNGUZA KUTUMIA WAZEE WASHAURI KWENYE KESI

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama, Bunda

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema Mahakama inakusudia kupunguza kuwatumia wazee washauri wa Mahakama katika kuamua mashauri Mahakamani na itabaki ikiwatumia katika mashauri ambayo yataonekana yana ulazima wa kuwatumia wazee hao.

Akizungumza wilayani Bunda ambapo ameanza ziara ya kikazi kukagua shughuli za Mahakama katika Mkoa wa Mara, Jaji Kiongozi amesema wazee hao watatumiwa na Mahakama kwenye mashauri ambayo yatakuwa na ulazima wa kuwatumia lakini yale ambayo siyo lazima, wazee hao wataacha kutumiwa.

Jaji Kiongozi amesema baadhi ya wazee washauri wa Mahakama hujishirikisha na vitendo vya rushwa na wakati mwingine huwatisha Mahakimu wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao.

Alisema matumizi ya wazee washauri wa Mahakama wakati mwingine husababisha mashauri kuchelewa kumalizika kutokana na kuchelewa kwao kufika Mahakamani na kusababisha mashauri kutokusikilizwa kwa wakati.

Akizungumza kuhusu rushwa, Mhe. Dkt, Feleshi alisema Mahakama kama Taasisi  haijishirikishi na vitendo vya rushwa bali vitendo hivyo hufanywa na  baadhi ya watumishi wasio waaminifu ndani ya Mahakama.

“Tuachane na maneno mepesi mepesi kuhusu rushwa kwa kuwa taarifa zipo, pelekeni Takukuru, hakuna anayemlinda mtu”, alisema Jaji Kiongozi.

Alisema Mahakama itashirikiana na Serikali katika kupambanana na rushwa na hivvo aliwataka wananchi wenye taarifa juu ya vitendo hivyo kuwasilisha kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa –Takukuru.

Aidha, Mhe. Dkt. Feleshi amesema Mahakama na Serikali katika wilaya ya Bunda wanapaswa kushirikiana katika kutatua changamoto nyingine mbalimbali za wananchi kwa kuwa wote wanamtumikia mwananchi.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Bunda, Jaji Kiongozi amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kubeba matarajio ya Taasisi kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aliwataka Mahakimu kumalizika mashauri kwa wakati, pamoja na kutoa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri ndani ya muda uliopangwa ambao kwa nakala za hukumu ni siku 21 tangu kumalizika kwa shauri na mienendo ya shauri hutolewa ndani ya siku 30.

Aidha, aliwataka watumishi hao kujenga tabia ya kutafuta na kufahamu taarifa mbalimbali za Mahakama kupitia Tovuti pamoja na Blog ya Mahakama ya Tanzania.

Naye Mkuu wa wilaya ya Bunda Bibi Lydia Bupilipili amewashauri Watumishi wa Mahakama kujenga mazingira yatakayowafanya wananchi kuendelea kuiamini Mahakama ya Tanzania kwa kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi.

Alisema Serikali pamoja na Mahakama wilayani Bunda wanashirikiana katika kutatua baadhi ya changamoto za Mahakama huku akitoa wito kwa Mahakimu kutumia njia ya usuluhishi katika kutatua baadhi ya migogoro miongoni mwa wananchi.

Mkuu huyo wa wilaya pia aliishauri Mahakama ya Tanzania kujikita katika kutoa elimu kwa wananchi hasa kwenye maeneo yenye changamoto zaidi wakati wa maadhimisho ya wiki ya sheria ambayo hufanyika kila mwaka nchini.

Alisema wananchi hawana budi kufahamu taratibu mbalimbali za Mahakma hususan zile za ufunguaji wa mashauri Mahakamani.

Jaji Kiongozi ameanza ziara ya kikazi ya siku tano Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma ambapo atakagua shughuli mbalimbali za Mahakama katika wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime pamoja na Musoma.

Comments (1)

  • Photo Loading... Elikana Teonest

    Ni sahihi kwa kiasi chake kwani hadi hivi sasa mashauri mengi ya Mahakama za Mwanzo yanachelewa kutolewa maamuzi kwa wakati kutokana na kutohudhuria kwa wazee wa Mahakama. ni vyema sasa Sheria ya Mahakimu (MCA), 1963 ifanyiwe marejeo ili kukidhi mahitaji ya haki za wateja wa Mahakama, tukikumbuka "THE CASE DELAYED IS THE JUSTICE DENIED". ninakushukuru Mhe. Dkt, jaji kiongozi kwa kuitambua changamoto hii.

    21-10-2019

Leave a Comment