Post Details

MTENDAJI MKUU AMUELEKEZA MKANDARASI KUKAMILISHA HARAKA JENGO LA MAHAKAMA -MANYARA

Published By:Mary C. Gwera

Mtendaji Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga amefanya ukaguzi katika jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na kuridhishwa na hatua ya jengo hilo lilipofikia na kumuhimiza Mkandarasi kulikamilisha mapema iwezekanavyo.

Akikagua jengo hilo mapema Oktoba 06, 2019, Bw. Kattanga alisema, “hatua ya jengo lilipofikia ni nzuri, hata hivyo natoa rai kwa Mkandarasi kukamilisha marekebisho madogo yaliyotolewa ili kazi za Mahakama ziendelee.”

Pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Wajumbe wengine walioambatana nae katika ukaguzi huo ni pamoja na Mhandisi Mkadiriaji Majengo kutoka Mahakama ya Tanzania, Bw. Raphael Bandiho, Wakandarasi wa jengo hilo kutoka Kampuni ya Vumwe General Services and Supplies Limited (VGSS), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)- Mkoa wa Manyara.

Wengine ni Wasimamizi na Washauri katika mradi huu, TEMESA-Mkoa wa Manyara pamoja na wenyeji ambao ni Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Manyara, Bw. Jacob Swalle, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Manyara, Mhe. Simon Kobero na Afisa Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Bw. Christopher Msagati.

Kwa kipindi kirefu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara ilikuwa ikitumia jengo la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM- Manyara) wakati wakisubiri jengo hilo la Mahakama likamilike.

Aidha; ilipofika mwezi Agosti mwaka huu shughuli za kuhamia katika jengo hilo jipya zilianza rasmi na walihamia katika upande mmoja wa Jengo ambao tayari ulikuwa umekamilika wakati Mkandarasi akiendelea kukamilisha upande mwingine wa jengo.

Inatarajiwa kuwa mradi wa jengo hili utakamilika hivi karibuni ndipo likabidhiwe rasmi kwa Mahakama kuendelea na shughuli zake kikamilifu.

Comments (0)

Leave a Comment