Post Details

JAJI MUNISI: FANYENI KAZI KWA BIDII KUWEZESHA UTOAJI HAKI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ama – Isario Munisi amewataka Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kufanya kazi kwa bidii ili kuwezesha upatikanaji na utoaji haki kwa wakati.
 
Akizungumza na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,wakiwemo watumishi wengine wa mahakama hiyo, wakati wa hafla ya kumwuaga kitaaluma iliyofanyika leo katika ukumbi wa Mahakama Kuu, jijini Dar es Salaam, Jaji Munisi alisema kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ndio msingi wa mafanikio katika utendaji kazi.
 
“Mnatakiwa kufanya kazi wa bidii ili kuweza kumaliza shughuli kwa wakati na kwa usahihi,pia mnapofanya kazi mnatakiwa kujiamini na kuaminiana,” alisema Jaji Munisi.
 
Aliongeza kuwa watumishi hao, wanatakiwa kuipenda kazi na kuwapenda watu wanofanya nao kazi ili kuweza kutimiza majukumu mbalimbali.
 
Aliwataka watumishi hao, kuwa wanapofanya kazi kwa bidii, pia wakumbuke kuwa kuna muda wa kupumzika.
 
Jaji Munisi alitumia nafasi hiyo,pia kumshukuru Jaji Kiongozi, Majaji wengine na watumishi aliofanya nao kazi, huku akisema kwamba amejifunza mengi kutoka kwao.
 
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi alisema Jaji Munisi aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2010, alikuwa ni mtu mbunifu katika kazi yake na aliweza kufanya kazi katika majukumu mbalimbali nchini.

Alitaja miongoni mwa majukumu hayo kutoa uzoefu wa utendaji kazi katika masuala ya sheria za makosa ya jinai na Haki za Binadamu.
 
Aidha Jaji Munisi aliajiriwa rasmi kuwa Wakili wa Serikali Daraja la III mwaka 1984.
 
Naye Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pia ni Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Ephery Sedekia, alisema kwa kipindi cha miaka tisa ya ujaji wake, Jaji Munisi ameweza kutoa mchango katika kuendeleza sheria mbalimbali, zikiwemo za madai,jinai,utawala na Katiba.

Comments (0)

Leave a Comment