Post Details

JAJI MAGHIMBI AWAPONGEZA WATUMISHI DIVISHENI YA KAZI KWA USHIRIKIANO

Published By:Mary C. Gwera

 Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi amewapongeza Watumishi kwa kufanya kazi kwa ushirikiano ulioiwezesha Mahakama hiyo kufanikiwa kuondosha mlundikano wa mashauri.

Akizungumza na Watumishi hao alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama hiyo jana tarehe 12 Mei, 2022 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Kinondoni jijini Dar es Salaam. Mhe. Maghimbi alisema ushirikiano ni chachu ya mafanikio katika kazi.

Kwa mujibu wa takwimu za Mahakama hiyo, zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2020 hadi sasa mwaka 2022 Divisheni hiyo imesikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 3,393 kati ya mashauri 5307 yaliyosajiliwa.

 “Kipekee napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa kujituma kwenu, hadi kuiwezesha Divisheni yetu kuwa katika nafasi nzuri ya kutokuwa na mlundikano wa mashauri kama ilivyokuwa awali na hata kuiwezesha Mahakama yetu kung’aa,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.

 Mhe. Maghimbi alisema kuwa kufanyika kwa Baraza la Wafanyakazi ni alama ya kuonyesha na kutambua juhudi zinazofanywa na Wafanyakazi katika kutekeleza majukumu. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha mahitaji ya Watumishi yanafanyiwa kazi ipasavyo kwa kushughulikia hoja zote zinazowasilishwa na wajumbe wa kikao.

“Kufanyika kwa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ni utekelezaji wa Sera ya ushirikishwaji wafanyakazi katika Uongozi wa pamoja mahali pa kazi; kama ilivyo katika Sheria ya Utumishi wa Umma sura 298 ya mwaka 2002, kanuni ya 108 ya kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, kifungu cha 30 (3) cha Sheria ya majadiliano ya pamoja Na. 19, Kanuni ya 24 ya kanuni za Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005 na Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini Na. 6 kifungu cha 73 (1) (2) (3),” alieleza.

Aidha Mwakilishi wa Watumishi kutoka Divisheni hiyo, Bi. Amina Ngonyani aliainisha hoja mbalimbali za Watumishi katika kikao hicho ikiwa ni pamoja na kupandishwa vyeo na mishahara, kupatiwa mafunzo na nyinginezo.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Wafanyakazi wa Divisheni hiyo pamoja na Katibu wa TUGHE, Mahakama ya Tanzania, Bw. Michael Masubo ulifanyika pia uchaguzi wa Katibu na Naibu Katibu ambapo aliyeshinda nafasi ya Katibu wa Baraza hilo ni Bi. Beatrice Silidion na Naibu wake akiwa Robert Mchocha.

Mada mbalimbali zilijadiliwa katika kikao hicho ikiwa ni pamoja na kujadili bajeti ya Divisheni ya Kazi ya mwaka wa fedha 2022/2023 lengo likiwa ni kuwa na uelewa wa pamoja katika mipango na matarajio ya matumizi ya fedha tunazopokea kwa ajili ya uendeshaji wa Mashauri na shughuli za Ofisi.

Ajenda nyingine ilikuwa kupokea taarifa fupi ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2020/2021 – 2024/2025 na mipango ambayo Mahakama imeweka kwa ajili ya Wafanyakazi kwa lengo la kuboresha Maslahi ya Watumishi, mifumo ya Tehama na utoaji haki kwa wakati.

Comments (0)

Leave a Comment