Post Details

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA ACHARUKA UCHELEWESHAJI MIRADI YA UJENZI

Published By:LYDIA CHURI

  • Amtaka Mkandarasi ujenzi Mahakama ya Wilaya Busega kukamilisha kazi mwezi ujao

Na. Emmanuel Oguda – Mahakama, Shinyanga

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameendelea na ziara yake ya kikazi kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama ambapo jana tarehe 10 Mei, 2022 alikagua mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Busega na kuwataka wakandarasi kukamilisha mradi huo mwezi ujao.

Prof. Ole Gabriel amesema wakandarasi ‘United Bulders Limited (UBL)’ wanaotekeleza mradi wa Mahakama hiyo inayojengwa katika Makao Makuu ya Wilaya yaliyopo katika Kata ya Nyashimo, mkoani Simiyu wanatakiwa kukamilisha kazi hiyo kabla ya tarehe 30 Juni, 2022 na hapatakuwepo na nyongeza ya muda wa ziada.

Mtendaji Mkuu huyo amesema alipotembelea mradi wa ujenzi huo kuwa wakandarasi wazawa wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kukamilisha kwa wakati miradi wanayopewa, jambo ambalo litaongeza tija na uaminifu katika mikataba wanayoingia na taasisi za Serikali.

Prof. Ole Gabriel ameahidi kutembelea maeneo mengine ambayo Mahakama ya Tanzania inatekeleza miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya ikiwemo Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu.

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu amewataka watumishi wote kuitunza na kuilinda miundombinu ya Mahakama pamoja na rasilimali fedha ili kuongeza tija katika kutoa haki kwa wananchi kwa wakati.

Kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Busega kutapunguza kwa kiwango kikubwa gharama kwa wananchi ambao hulazimika kusafiri umbali wa kilometa 120 kutoka Busega hadi Bariadi na kutumia kati ya shilingi 30,000 za Kitanzania kama gharama za nauli kwenda na kurudi hadi shilingi 50,000 za Kitanzania anapolazimika kulala Bariadi ili kuhudhuria shauri lake mahakamani.

Ujenzi wa Mahakama hiyo ya Wilaya unalenga kusogeza huduma kwa wananchi pamoja na kuondoa gharama za usafiri na malazi  wanapohudhuria mashauri yao ambayo kwa sasa husikilizwa katika Mahakama ya Wilaya Bariadi.

Comments (0)

Leave a Comment