Post Details

WATUMISHI WA MAHAKAMA YA TANZANIA WAPIMA HOMA YA INI

Published By:Mary C. Gwera

Daktari Bingwa wa Virusi vinavyosababisha Saratani ambaye pia ni mtafiti anayefanya tafiti za seli za saratani kutoka Taasisi ya Saratani ‘Ocean Road’, jijini Dar es Salaam, Kandali Samweli, amewataka watumishi wa Mahakama ya Tanzania kujitokeza
mapema kuchunguza afya zao na kupata chanjo dhidi ya maambukizi ya homa ya Ini ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo. 

Wito huo umetolewa, leo Septemba 19, 2019 na Daktari huyo wakati wa utoaji elimu, upimaji hiari na utoaji chanjo dhidi ya homa ya Ini kwa watumishi hao, kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, unaoendelea kufanyika kwa muda wa siku tatu katika ukumbi wa Mahakama Kuu, uliopo jijini Dar es Salaam, ambapo takribani watumishi 170 wanatarajiwa kufanyiwa kipimo cha ugonjwa huo kwa hiari.

Akizungumza na watumishi hao, mahakamani hapo, Dkt, Samweli, amesema chanjo hiyo hutolewa kwa awamu tatu, ambapo ya kwanza hutolewa mara baada ya kipimo cha Hepatitis B, ya pili hutolewa mwezi mmoja baada ya chanjo ya kwanza, na chanjo ya tatu hutolewa miezi sita baada ya chanjo ya kwanza.

Dkt. huyo alieleza kuwa katika makundi ya virusi vya ‘Hepatitis’ A, B, C na D homa ya ini husababishwa na kirusi aina ya ‘Hepatitis B’. Hivyo tafiti zinaonyesha kwamba mtu mmoja kati ya ishirini ana maambukizi ya ‘Hepatitis B’.

 Alifanunua  kuwa chanjo hiyo ilianza kutolewa kwa watoto mnamo mwaka 2002 ambapo chanjo hiyo huambatanishwa na chanjo nyingine zinazotolewa punde mtoto anapozaliwa.

‘Chanjo hii ilianza kutolewa mwaka 2002 kwa watoto na inaambatanishwa na chanjo nyingine kwenye kadi ya mtoto, hivyo wanaotakiwa kupata chanjo hii ni waliozaliwa mwaka 2001 na miaka ya nyuma, na tayari tumeshaanza kutoa chanjo hii kwa watu wengine.’ alisema Dkt. Samweli.

Alisema chanjo hiyo hutolewa kwa rika na jinsia zote, na ni salama kwa wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.

Alizungumzia kuhusu dalili za ugonjwa huo, alisema hazionekani kwa urahisi kwani hujitokeza baada ya muathirika kuathirika kwa muda mrefu.

Alizitaja baadhi ya njia zinazoweza kusababisha maambukizi ya ugonjwa huo, kuwa ni kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua, mgusano baina ya mtu na mtu kupitia damu na majimaji mengine ya mwili, ngono zembe, kuchangia vitu vyenye ncha kali na mtu mwenye virusi hivyo na kuongezewa damu iliyoathiriwa na virusi hivyo.

Aidha jamii inatakiwa kuchunguza afya zao kwa kupata kipimo hicho, ikiwemo chanjo mapema kwani mtu anaweza kupata virusi hivyo bila dalili kujitokeza, kwani dalili zinajitokeza baada ya madhara makubwa,’ alisisitiza huku akisema athari za kuishi na virusi vya Hepatitis B pasipo tiba huweza kusababisha Saratani ya Ini.

Kwa upande wake Naibu Msajili Mahakama Kuu, Mhe. Devotha Kamuzora, amesema kuwa huduma hiyo ya utoaji chanjo dhidi ya homa ya ini ni nzuri na imerahisishwa kwa kuletwa karibu yao kwani imewasaidia watumishi kujua hali zao juu ya ugonjwa huo, pia kuchukua tahadahari dhidi ya maambukizi.

Comments (0)

Leave a Comment