Post Details

TANZANIA YA KWANZA KUTOA HUDUMA, MAHAKAMA INAYOTEMBEA

Published By:Mary C. Gwera

Tanzania imetajwa kuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuanzisha huduma ya Mahakama inayotembea ‘Mobile Court’ lengo likiwa ni kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi.

Mtaalam Mwelekezi kutoka Benki ya Dunia, Bw. Waleed Malik alibainisha hayo Septemba 02, 2019 katika Kituo cha Mafunzo na Habari kilichopo eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu-Dar es Salaam wakati akitoa Mada katika Mafunzo kwa vitendo kwa baadhi ya Watumishi wa Mahakama wa jijini Dar es Salaam wanaohudumu katika Mahakama hiyo.

“Kwa kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza katika Bara la Afrika kuanzisha huduma hii ni vyema mkatoa huduma bora zenye viwango ili nchi nyingine zivutiwe na kuja kujifunza kutoka kwenu,” alieleza Bw. Malik.

Aidha; Mwezeshaji huyo wa Mafunzo hayo kutoka Benki ya Dunia, aliwasisitiza Watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano ‘team work’ kwa kuwa ndio nguzo kuu ya mafanikio.

“Nawaomba kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta matokeo chanya ya huduma hii,” alisema Bw. Malik.

Aidha; Mtaalam huyo pia alisisitiza juu ya utoaji elimu kwa umma kuhusu Mahakama hiyo ili jamii iwe na uelewa wa jinsi inavyofanya kazi na huduma inazotoa.

Akifungua rasmi Mafunzo hayo, naye Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati amewaasa Watumishi wanaofanya kazi katika Mahakama hiyo kutojihusisha na vitendo vya rushwa pindi wanapotekeleza majukumu yao.

 “Mahakama imewaamini ninyi, na mpo katika historia ya kuwa sehemu ya Watumishi wa kwanza kutoa huduma katika aina hii ya Mahakama, hivyo ni rai yangu kwenu kutojihusisha na vitendo hivyo kwakuwa vitaidhoofisha Mahakama kwa ujumla,” alisisitiza Mhe. Revocati.

Mbali na vitendo vya rushwa, Mhe. Msajili Mkuu vilevile alisisitiza juu ya kutoa huduma nzuri kwa wateja ‘customer care’ ili lengo kuu linalokusudiwa na Mahakama ya Tanzania la utoaji huduma bora kwa wananchi liweze kufikiwa.

Jumla ya Washiriki 50 ambao ni Mahakimu, Dereva, Washauri wa Mahakama, Makarani wa Mahakama, Maafisa Utumishi na Utawala, Maafisa Habari, Makatibu Muhtasi pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wameshiriki katika mafunzo kwa vitendo kuhusiana na utoaji huduma ya Mahakama inayotembea ikiwa ni kuwawezesha kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.

Kwa sasa Mahakama zinazotembea zipo mbili na zinatoa huduma katika mikoa miwili ya Dar es Salaam na Mwanza, hata hivyo; Mahakama ya Tanzania ina mpango wa kutanua wigo wa utoaji huduma hii kwa kuanzisha vituo vingine katika mikoa iliyosalia kwa awamu tofauti kulingana na upatikanaji wa fedha.

Baadhi ya nchi nyingine zinazotoa huduma ya Mahakama inayotembea ni pamoja na Guatemala, Brazil na Pakistan.

Comments (0)

Leave a Comment