Post Details

JAJI MATUMA ATOA WITO MUHIMU KWA WAPELELEZI

Published By:LYDIA CHURI

Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma amewataka maafisa upelelezi ndani ya Kanda hiyo kukamilisha upelelezi kwa haraka ili mashauri ya jinai yaliyopo mahakamani yamalizike kwa wakati.

Mhe. Matuma alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na maafisa upelelezi kutoka Mikoa ya Shinyanga na Simiyu tarehe hivi karibuni.

Jaji Mfawidhi huyo aliwahimiza maafisa hao kutoka Jeshi la Polisi kuchuja vielelezo na ushahidi unaowasilishwa mahakamani ili kuondoa mashaka yanayoweza kujitokeza wakati wa usikilizaji wa mashauri hayo.

“Wapo baadhi ya wapelelezi huchelewesha upelelezi kwa makusudi na kusababisha shauri kukaa mahakamani kwa muda mrefu hata zaidi ya miaka mitatu. Wapelelezi wa namna hii hatutawavumilia katika Kanda yetu ya Shinyanga,” alionya Mhe. Matuma.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwasisitiza maafisa hao wa upelelezi na Mahakimu wote wa Kanda ya Shinyanga kuhakikisha watuhumiwa ambao wanadhaminika na waliotimiza masharti ya dhamana wanapewe dhamana ili kuondoa mlundikano wa mahabusu Magereza.

“Wapo baadhi ya askari wapelelezi kwa kushirikiana na baadhi ya Mahakimu wamekuwa wakizuia dhamana kwa watuhumiwa ambao wanastahili kupewa dhamana. Ni heri kuwaachilia huru watu mia moja wenye hatia kuliko kumtia hatiani mtu mmoja asiye na hatia,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mhe. Matuma amewapongeza maafisa wa TAKUKURU kwa kufanfanya kazi zao kwa umakini na kwa weledi. “Niwapongeze TAKUKURU, nimefanya kazi nao muda mrefu wanawasilisha ushahidi na vielelezo vilivyojitosheleza, niwaombe muendelee na kazi hiyo nzuri,” aliongeza.

Kikao hicho ni muendelezo wa vikao kazi kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga pamoja na wadau wanaofanya kazi kwa karibu na Mahakama katika kutatua changamoto mbalimbali ili kushirikiana pamoja katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2020/21 – 2024/25.

Comments (0)

Leave a Comment