Post Details

MAHAKAMA YA TANZANIA YAANZISHA KITUO CHA HUDUMA KWA MTEJA

Published By:LYDIA CHURI

Na. Faustine Kapama-Mahakama, Songea.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 1 Machi, 2022 ametangaza kuanzishwa kwa kituo kipya cha Huduma kwa Mteja, ‘Call Centre’ kinachowezesha wananchi kupiga simu masaa 24 ili kujua huduma zote zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania.

Habari hizo njema zimetangazwa na Mhe. Prof. Juma alipokuwa anaongea na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Dkt. Julius Ningu alipomtembelea ofisini kwake katika siku yake ya pili ya ziara ya kikazi ya kimahakama, Kanda ya Songea. Amesema kuwa Kituo hicho kimeanza kufanya kazi leo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni ambapo mwananchi akipiga simu atajibiwa hapo hapo.

 “Tunawaomba wananchi wasilalamike sana, wafikishe malalamiko yao na sisi tutayashughulikia. Tunawaomba watusaidie kuifahamu  Mahakama. Kwa mfano, hata mimi naweza pengine siifahamu Mahakama vizuri kwa sababu sina uwezo wa kujua yanayotokea katika Mahakama za Mwanzo zilizo mbali. Lakini mwananchi ambaye anatafuta zile huduma atakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi,” amesema.

Jaji Mkuu pia alimweleza Mkuu huyo wa Wilaya kuwa Mahakama ya Tanzania inathamini sana mrejesho kutoka kwa wananchi kwa vile huduma ya Mahakama ni huduma ya umma. Alisisitiza kuwa licha ya kulalamikiwa, lazima Mahakama inatakiwa kusikiliza na kushughulikia suala linalolalamikiwa.

“Tumetoa utaratibu wa kupokea hayo malalamiko ambao tunauita mrejesho wa huduma kwa mteja. Fomu za mrejesho huo zipo kwenye tovuti ya Mahakama. (Fomu hizo) zinaainisha namna ya kuzijaza ili kujua nani anayelalamikiwa, hatua itakayowezesha uongozi wa Mahakama kujua tatizo lilipo,” Mhe. Prof. Juma amesema.

Alitoa mfano fomu hiyo inauliza jina la Mahakama inayolalamikiwa, ngazi ya Mahakama, kama ni Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi  au Mahakama Kuu. Pia fomu hiyo inauliza kama mwananchi anakumbuka namba ya kesi yake na ni namba ngapi, nani unayemlalamikia, kama ni Jaji, Hakimu, Karani, Mtendaji au Mlinzi maana wakati mwingine mtu anaweza kukutana na mlinzi na asipopata huduma nzuri huondoka na picha hasi dhidi ya Mahakama yote kuwa haitoi huduma nzuri kwa wananchi.

“Hivyo, hizi fomu zinatusaidia sana sisi kujua lalamiko lako ni nini, (kama ni) usikilizaji wa shauri, kuchelewa kupata nakala ya hukumu au hukumu imeahirishwa mara kwa mara, amri ya Mahakama haitekelezwi au kuna huduma nyingine ambayo unaona wewe inakugusa (kama)  mwananchi. Sisi tunaona siyo vizuri kwa mwananchi kuwa analalamika tu, lakini lalamiko lake halipatiwi ufumbuzi,” amesema.

Baada ya kuongea na Mkuu wa Wilaya, Dkt. Ningu, ambaye aliisifia Mahakama ya Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya kwa wananchi, Jaji Mkuu alitembelea mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo ambalo litagharibu zaidi ya millioni 630 za Kitanzania. Utekelezaji wa mradi huo ulianza tarehe 18 Februari, 2021 na unatarajia kukamilika tarehe 16 Agosti 16, 2022.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Bw.  Geofrey Mashafi alitoa taarifa fupi ya ujenzi inayoonyesha kuwa hadi sasa Mkandarasi M/S Moladi Tanzania Limited ameshalipwa zaidi ya millioni 420 za Kitanzania kwa ajili ya kazi alizotekeleza. Alisema ujenzi wa msingi, tofali, kupiga lipu, kuezeka bati, kuweka ceiling board na upigaji rangi katika jengo kuu la Mahakama na choo cha nje umeshakamilika na kwamba uwekaji wa milango na madirisha unaendelea.

Katika ziara yake ya siku nne, Jaji Mkuu atatembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru na kuhitimisha ziara hiyo kwa kutembelea Mahakama ya Wilaya Songea, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea na Mahakama Kuu Songea. Katika maeneo yote atakayopitia, Mhe. Prof. Juma atakagua shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuongea na watumishi wa kada zote.

Katika ziara hiyo, Jaji Mkuu ameambatana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha.

Wengine ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba, Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Katibu wa Msajili Mkuu, Bw. Jovin Constantine, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice Patrick na mwakilishi wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury.

Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Sekela Moshi, Naibu Msajili, Mhe. Warsha Ng’umbu, Mtendaji wa Mahakama Kuu wa Kanda, Bw.  Geofrey Mashafi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Songea, Mhe. Livin Lyakinana, Afisa Utumishi, Bw. Brian Haule, Mhasibu, Bw. Japhet Komba na Afisa TEHAMA, Bi. Catherine Francis.

Comments (0)

Leave a Comment