Post Details

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA AKUTANA NA VIONGOZI WA JUMUIYA YA MARIDHIANO

Published By:Mary C. Gwera

Na Mary Gwera, Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 04 Desemba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania na kuahidi kushirikiana nao katika kutatua migogoro mbalimbali.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika kwenye Ofisi ya Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, Prof. Ole Gabriel alisema kuwa lengo la ujio wa Viongozi hao ni kufahamiana pamoja na kushirikiana katika kuendeleza maridhiano hata katika ngazi ya Mahakama.

“Kwanza napenda kuwashukuru kwa kututembelea na pia kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuwaombea Viongozi wa Taifa hili kuendelea kudumisha amani,” alisema Mtendaji Mkuu.

Alisema pia, suala la maridhiano ni la msingi kwakuwa linahitajika hata kwa Mahakama, ambapo amewaomba Viongozi hao wa dini kuwaeleza Waumini kupitia kanisani na misikitini kuhusu umuhimu wa maridhiano badala ya kufikishana mahakamani hata kwa makosa ambayo yanasameheka na kuongeza kuwa waumini wanatakiwa kuwa na utii wa sheria bila shuruti.

Aidha, Mtendaji Mkuu aliongeza kuwa, Mahakama itajipanga kwa kutoa mafunzo maalum kwa viongozi hao ili waweze kupata elimu zaidi ya masuala ya usuluhishi na maridhiano ili wanapotoa elimu kwa umma wawe na ufahamu zaidi kuhusu suala la usuluhishi na maridhiano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Shekhe Alhad Mussa Salum alisema kuwa Jumuiya hiyo imejikita katika kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kudumisha amani na utulivu, kushughulikia/kusuluhisha migogoro mbalimbali ya Taasisi kwa Taasisi na pengine ya watu ili waweze kufikia muafaka kwa njia ya kusameheana kiiamani.

“Tunashughulika na migogoro mbalimbali hata migogoro ya mtu kwa mtu, chombo na chombo, Taasisi, Jumuiya vyote tunaweza kusaidia kwa njia rahisi zaidi kupitia mafundisho ya dini zetu,” alisema Shekhe Salum.

Mazungumzo hayo yaliyohusisha pande zote mbili za Mahakama na Jumuiya hiyo yalihudhuriwa pia na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Anatory Kagaruki, Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw. Allan Machella.

Kwa upande wa Jumuiya ya Maridhiano viongozi walioambatana pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ni Katibu Mkuu wa Jumuiya, Askofu Dkt. Israel Maasa na Naibu Katibu wa Jumuiya hiyo, Shekhe Dkt. Abdulrazak Juma.

Comments (0)

Leave a Comment